IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Waliomuua shahidi Fakhirzadeh wapewe adhabu, jitihada zake ziendelee

19:43 - November 28, 2020
Habari ID: 3473403
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametilia mkazo wajibu wa kutiwa adabu na kupewa adhabu isiyoepukika wote waliofanya na kuamrisha mauaji ya kigaidi ya mwanasayansi wa Kiirani, Dk. Mohsen Fakhrizadeh.

Mapema leo asubuhi, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametuma ujumbe wa pongezi na tanzia kufuatia kuuawa shahidi na kumpoteza mwanasayansi bingwa aliyebobea katika masuala ya nyuklia na ulinzi wa Iran, Dk Mohsen Fakhrizadeh na amesisitiza kutolewa adhabu isiyoepukika kwa waliofanya na walioamrisha jinai hiyo na wajibu wa kuendelezwa jitihada za kielimu na kiufundi za shahid Fakhrizadeh.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema katika ujumbe wake huo kwamba: Mwanasayansi huyu bingwa wa nyuklia na masuala ya ulinzi ambaye ameuliwa shahidi na mamluki watenda jinai na wenye nyoyo ngumu, ametoa roho yake azizi na yenye thamani kubwa katika njia ya Allah kupitia jitihada zake kubwa za kielimu na za kubakia milele na hivyo amefanikiwa kupata daraja ya juu ya kuuawa shahidi ikiwa ni zawadi kutoka kwa Mola wake.

Mohsen Fakhrizadeh, Mkuu wa Shirika la Utafiti na Ubunifu la Wizara ya Ulinzi ya Iran aliuawa shahidi jana jioni katika shambulio la kigaidi lililofanywa katika viunga vya jiji la Tehran.

Kwa upande wake, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, maadui wote watambue kwamba, wananchi na viongozi wa Iran ni mashujaa na wenye ghera kubwa, hivyo lazima watalipiza kisasi cha vitendo vya jinai linavyofanyiwa taifa hili la Kiislamu.

Rais Hassan Rouhani amesema hayo leo Jumamosi katika kikao cha Kamati ya Taifa ya Kukabiliana na Ugonjwa wa Corona ikiwa ni kuonesha hisia zake baada ya maadui kumuua kigaidi mwanasayansi mkubwa wa Iran, Mohsen Fakhrizadeh na kusisitiza kukwa, ugaidi huo wa kinyama umeonesha kwamba maadui wa Iran ya Kiislamu wanapitia wiki nzito sana, wiki ambayo wanahisi hali duniani inazidi kubadilika dhidi yao na kwao wao ni muhimu sana kutumia wiki chache zilizobakia kutenda jinai kubwa kadiri wanavyoweza.

Kabla ya hapo pia Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa, maadui woga wa taifa wa Iran wajue kwamba kumuua shahidi Mohsen Fakhrizadeh hakutateteresha hata kidogo irada ya vijana na wanasayansi wa Iran ya Kiislamu ya kushikamana na njia ya ustawi wa kasi wa kielimu na kufikia kwenye vilele vya mafanikio ya kujivunia; lakini badala yake yatawafanya wawe na azma thabiti zaidi ya kuendeleza njia ya shahidi huyo mwenye hadhi kubwa; na damu za mashahidi wa Iran zitaendelea kubakia zikichemka na kutiririka.

Mbali na masuala ya nyuklia na ulinzi, shahid Fakhrizadeh alikuwa mstari wa mbele pia katika kupambana na ugonjwa wa corona kiasi kwamba, kifaa cha kwanza kabisa cha kuchukulia vipimo vya COVID-19 nchini Iran kilibuniwa na kuundwa na taasisi aliyokuwa akiiongoza yeye.

3937799

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha