IQNA

Ayatullah Isa Qassim: Ukandamizaji umeifanya Bahrain kuwa sawa na gereza kubwa

11:54 - January 07, 2021
Habari ID: 3473533
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini Bahrain amesema kuwa dhulma na ukandamizaji unaofanywa na utawala wa ukoo wa Aal Khalifa dhidi ya taifa la Bahrain umeifanya nchi hiyo kuwa sawa na gereza kubwa

Taarifa iliyotolewa na Ayatullah Sheikh Isa Qassim imesema kuwa, gereza kubwa la Bahrain limejaa gereza ndogo ndogo ambazo mahabusu na wafungwa wake wanashikiliwa kwa sababu tu ya kupinga siasa za utawala wa nchi hii.

Sheikh Isa Qassim ameongeza kuwa, kuna ulazima wa kusikilizwa sauti ya wananchi wa Bahrain kwa ajili ya kuainisha mustakbali wa nchi yao na kuheshimiwa matakwa na irada yao; kwani utawala wowote hauwezi kubakia madarakani bila ya kutilia maanani matakwa ya wananchi.

Tangu Februari mwaka 2011, wakati ulipoanza mwamko wa Kiisamu Asia Magharibi, Bahrain imekuwa uwanja wa maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Khalifa.

Wananchi hao wanataka kuwepo uhuru, utekelezwe uadilifu, ukomeshwe ubaguzi na kuundwa serikali itakayochaguliwa na wananchi wenyewe.

Hata hivyo kwa msaada wa wanajeshi wa Saudi Arabia na askari usalama wa Imarati waliotumwa nchini Bahrain kupitia mpango wa ulinzi wa Ngao ya Kisiwa, utawala wa Aal Khalifa unatumia mkono wa chuma kukabiliana na matakwa ya wananchi hao.

Kwa mujibu wa duru za haki za binadamu, Bahrain ina idadi kubwa zaidi ya wafungwa wa kisiasa kulinganisha na idadi ya watu katika nchi hiyo ndogo zaidi katika Ghuba ya Uajemi.

3946200

captcha