IQNA

Bango la Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Iran lazinduliwa

21:03 - February 21, 2021
Habari ID: 3473670
TEHRAN (IQNA) – Bango la Mashindano ya 37 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu limezinduliwa wiki mbili kabla ya kuanza mashindano hayo.

Juu ya Bango hilo kuna maandishi yenye kauli mbiu ya mashindano ya mwaka huu ambayo ni "Kitabu Kimoja, Ummah Mmoja."

Bango hilo lina picha ya mabara yote matano ya dunia na pia maelezo kuhusu mashindano hayo.

Fainali ya Mashindano ya 37 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Iran itafanyika kuanzia Machi 6 hadi Machi 11.

Kutokana na maambukizi ya COVID-19 au corona duniani kote, mashindano ya mwaka huu yatafanyika kwa njia ya mawasiliano ya video kupitia intaneti.

Washindani 120 kutoka nchi 70 walishiriki katika nusu fainali ya mashindano hayo iliyofanyika kwa njia ya intaneti pia mwezi uliopita. Mchujo wa mashindano hayo ulikuwa na washiriki 600 kutoka nchi 70.

Kwa mujibu wa kamati ya majaji wa mashindano ya mwaka huu, wasomaji Qur'ani (quraa) kutoka Indonesia, Iran, Iraq, Syria, Misri, na Lebanon  watashindana katika fainali ya kategoria ya Tahqiq huku katika kategoria ya Tarteel waliofika fainali wakiwa ni kutoka  Misri, Iran, Indonesia, Iraq, Algeria, Syria na Uholanzi.

Waliofika katika fainali katika kategoria ya kuhifadhi Qur'ani Tukufu kikamilifu ni kutoka Afrika Kusini, Russia, Afghanistan, Iran, Iraq, Marekani, Mauritania na Libya.

Aidha mbali na mashindano hayo ya kawaida kutakuwa na fainali za mashindano maalumu ya Qur'ani kwa ajili ya wanafunzi wa vyuo vya kidini na wanawake.

Shirika la Wakfu la Iran huandaa mashindano hayo ya kimataifa ya Qur'ani kila mwaka.

Kutokana na janga la COVID-19 mashindano hayo hayakufanyika mwaka 2020 na yalifanyika mara ya mwisho Aprili 2019 mjini Tehran ambapo washiriki kutoka nchi zaidi ya 80 walishiriki.

3955269

Kishikizo: mashindano ya qurani ، iran ، bango
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha