IQNA

Mkuu wa Kongamano la Kimataifa la Wauyghur katika mahojiano na IQNA

Serikali ya China inaendelea kuwakandamiza Waislamu wa jamii ya Uyghur

21:08 - February 21, 2021
Habari ID: 3473671
TEHRAN (IQNA) - Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kimataifa ya Jamii ya Uyghur Dolkun Isa anasema serikali ya China inaendeleza kampeni dhidi ya Waislamu wa jamii ya Uyghur kwa kisingizio cha kupambana na misimamo mikali ya kidini.

Katika fremu ya kampeni hiyo, mwaka 2016 kulianzishwa kambii kadhaa ambapo Waislamu wamepelekwa katika kambi ambako wanatumikishwa kwa nguvu. Anasema hivi sasa kuna Waislamu karibu milioni tatu katika kambi hizo ambapo wanakabiliwa na mateso makubwa.

Ili kufahamu zaidi kuhusu hali ya Waislamu wa jamii ya Uyghur nchini China, IQNA imefanya mahojiano maalumu na Dolkun Isa, Mwenyekiti wa wa Kongamano la Kimataifa la Wauyghur. Isa anafafanua kuhusu mateso ambayo Waislamu waliowachache wanapata mikononi mwa utawala wa China na anataka dunia na hasa nchi za Kiislamu zichukue hatua za kuishinikiza China isitishe hatua zake zilizo dhidi ya ubinadamu.

IQNA: Katika miaka ya hivi karibuni China imezidisha mashinikizo dhidi ya jamii ya Uyghur. Je chanzo cha kushinikizwa jamii  hii ya waliowachache hii ni nini hasa?

Isa: Kabla ya kujibu swali lako nataka kwanza kusema kuwa Wauyghur si wachache. Ukilinganisha idadi ya Wauyghur nchini China na wengine basi itakubainikia kuwa wengine ndio wachache. Pili tatizo la Wauyghur si jipya. Ni karibuni tu ndio dunia imeanza kulifahamu. Matatizo ya jamii hii yalianza mwaka 1949 wakati eneo la Turkestan Mashariki lilipopewa jina la Xinjiang na serikali ya China. Kimsingi eneo hilo lilikaliwa kwa mabavu na China ambayo ilidai hilo ni eneo lake la kale na huo ukawa mwanzo wa matatizo ya Wauyghur.

Mbali na kadhia ya Wauyghur, serikali ya China ilianza pia kutekeleza sera mpya kuhusu maeneo mengine kama vile Tibet na Mongolia. Tokea mwaka 2014, rais mpya wa China Xi Jinping alitupilia mbali sera za kujaribu kuwavutia Wauyghur upande wa serikali na badala yake akaanza kufuata sera ambayo tunaweza kuitaja kuwa ni ya maangamizi ya kimbari. Serikali ya China imechukua hatua kadhaa dhidi ya Wauyghur lakini inaficha vitendo vyake hivyo kwa sababu ni nchi kubwa na yenye uwezo mkubwa duniani. Aidha nchi nyingi duniani zinaitegemea China kiuchumi na hivyo zinapuuza ukiukwaji wa haki za binadamu nchini humo. Huu ndio ukweli wa mambo. Tokea mwaka 2016, serikali ya China ilianzisha kampeni dhidi ya Wauyghur kwa kisingizo cha kupambana na kile ilichodai kuwa ni ‘watu wenye misimamo mikali ya kidini’. Katika kampeni hiyo, Wauyghur zaidi ya milioni tatu Waislamu  wamewekwa katika kambi za kutumikshwa kwa lazima katika dunia ya leo ya karne ya 21.

اقدامات دولت چین علیه اویغورها جنگ علیه اسلام است

IQNA: Kwa hivyo kwa mtazamo wako, kupambana na misimamo mikali ni kisingizo kinachotumiwa kukabiliana na Waislamu?

Isa: Naam. Harakati au shughuli zote za kidini ni kinyume cha sheria. Hata kutamka maneneo ya kawaida  kama vile Asalam Aleikum, ambayo kimsingi ni salamu inayotumika na Waislamu wote duniani  ni kinyume cha sheria. Anayetumia salamu hii anatuhumiwa kuwa ni gaidi au mwenye misimamo mikali ya kidini.

IQNA: Yaani mtu anayetamka "Asalam Aleikum"  anapelekwa katika kambi ya kutumikishwa kwa nguvu. Una ushahidi wowote kuhusu hilo?

Isa: Naam. Hata ukipatikana na maandishi ya kidini unachukuliwa hatua. Maafisa wa usalama wanaweza wakakusimamisha na kuikagua simu yako ya mkononi na wakipata maandishi ya kidini hiyo inakuwa sababu tosha ya kufanya upelekwe katika kambi ya kutumikishwa kwa nguvu.

IQNA: Hali ya wanawake wanaovaa Hijabu ikoje?

Isa: Haiwezekani kuvaa Hijabu. Kuvaa aina yoyote ya Hijabu hata mtandio ambao haujafungwa vizuri ni kinyume cha sheria. Aidha ni kinyume cha sheria kufuga ndevu. Na yote hayo ni katika kisingizo cha kukabiliana na ‘misimao mikali ya kidini’. Hivi sasa hata Waislamu wanalazimishwa kula nyama ya nguruwe.

IQNA: Kinyume na inavyoshinikizwa serikali ya kijeshi hivi sasa nchini Myanmar, inaonekana serikali ya China haikabiliwi na mashinikizo ya nguvu kutoka  mashirika ya kutetea haki za binadamu duniani. Baadhi wanasema sababu ya hili ni uchumi mzuri wa China na uhusiano wake wa karibu na nchi za Kiislamu. Una mtazamo gani kuhusu nukta hii?

Isa: Inasikitisha kuwa aghalabu ya nchi za Kiislamu zimenyamazia kimya dhulma tunayotendewa. Kwa hakika kuhusiana na kadhia ya Waislamu Wauyghur, si tu kuwa nchi za Kiislamu zimekaa kimya, bali hata baadhi zinaiunga mkono serikali ya China.

Pamoja na hayo, Uhusiano wa Wairani na Wauyghur ni wa kihistoria na wa muda mrefu. Hata katika lugha yetu kuna maneno mengi ya Kifarsi kama vile Mungu (Khoda), mkate (Nan) na nyama (gosht). Takribani asilimia 20 ya maneneo ya lugha ya Uyghur yanatokana na ligha ya Kifarsi.

IQNA: Unatazama vipi mustakabali wa mateso dhidi Wauyghur na una matarajio yapi kutoka kwa serikali za dunia?

Isa: Lengo la serikali ya China ni hatari sana. Hii ni kwa sababu China inataka kuwaangamiza kikamilifu Waislamu Wauyghur au kuondoa kabisa utambulisho wao. Kwa kuwapiga marufuku kutumia lugha yao na kufuta mafundisho yao ya Kiislamu na pia utamaduni wao, China inataka kuwaangamiza Wauyghur. Serikali ya China imeanzisha kambi zinazoshabihiana na kambi za Vita Vikuu vya Pili vya Dunia ambapo Wauyughur wanalazimishwa kuishi hapo huku wanawake wakipewa dawa za kuwazuia kuzaa. Kwa hakika kinachojiri hapo ni utumwa mamboleo ambapo hata wazazi wanatenganishwa na watoto wao. Dunia haipaswi kukaa kimya mbele ya jinai za serikali ya China.

3955066

captcha