IQNA

22:33 - November 26, 2019
News ID: 3472232
TEHRAN (IQNA) – China imetoa taarifa na kupinga madai ya kimataifa kuwa imewaweka Waislamu wa mkoa wa Xinjiang katika kambi maalumu kwa lengo la kuwabadilisha itikadi zao.

Kupitia taarifa iliyotolewa Jumanne, Wizara ya Mambo ya Nje ya China imesema hakuna ukiukwaji wa haki za binadamu au ukandamizaji wa kikabila na kidini katika mkoa wa Xinjiang na kwamba oparesheni za usalama katika mkoa huo zinalenga kukabiliana na ‘utumiaji mabavu na ugaidi’.

Jibu hilo kali la Beijing linafuatia uvujaji mkubwa wa nyaraka za siri za serikali ya China ambazo zilichapishwa na Ubia wa Kimataifa wa Waandishi Habari Wapelelezi (ICIJ). Nyaraka hizo za siri zimebaini kuwa Waislamu zaidi ya milioni moja wa kabila la Uyghur nchini China wanashikiliwa na vikosi vya usalama katika kambi maalumu bila hatia au kufunguliwa mashtaka. 

Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya wataalamu wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa, Waislamu takribani milioni moja wa jamii ya Uighur wanashikiliwa katika kambi za kuwafunza Usosholisti wa Kichina kwa kisingizio cha kukabiliana na ugaidi.

Wizara ya Mambo ya China imetoa taarifa ndefu na kusema madai hayo hayana msingi na yanalenga kuharibi taswira ya nchi hiyo.

Aidha taarifa hiyo imesema sera za sasa za utawala katika mkoa wa Xinjiang zitaendelea kutekelezwa. Taarifa ya Wizara ya Mambo ya China hatahivyo haikutaja uwepo wa kambi hizo za kuwashikilia watu kwa nguvu na ambazo wakuu wa China wamekuwa wakisisitiza kuwa ni kambi za mafunzo ya kazi za utaalamu.

“Tokea mwaka 1990 hadi mwisho wa mwaka 2016, kumejiri matukio ya kigaidi katika mji wa Xinjiang na kusababisha watu wasio na hatia kupoteza maisha na mali kuharibiwa,” amesema Geng Shugan, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China katika taarifa iliyosambazwa na wizara hiyo.

Aidha ameongeza kuwa: “Kuna watu milioni 200 nchini China ambao wanafuata dini mbali mbali na miongoni mwao kuna Waislamu zaidi ya milioni 20 na kuna msikiti mmoja kwa kila Waislamu 530 mkoani Xinjiang.”

Amebaini zaidi kwa kusema: “Kuna misikiti 24,400 mkoani Xinjiang na kwa msingi huo ni wastani wa msikiti mmoja kwa kila Waislamu 530.”

Taarifa hiyo imebaini kuwa, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa amealikwa kutembelea mkoa wa Xinjiang.

3469973

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: