IQNA

Balozi wa Iran nchini China awatembelea Waislamu wa jamii ya Uighur

7:26 - March 31, 2021
Habari ID: 3473773
TEHRAN (IQNA)- Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko China jana Jumanne aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa ametembelea mkoa wenye Waislamu wengi nchini humo ambao wakaazi wake wengi Waislamu wa jamii wa Uighur.

Katika ujumbe wake huo, Balozi Mohammad Keshavarz-Zadeh amesema akiwa ameandamana na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai na mabalozi kadhaa wa nchi za kigeni wenye makao yao Beijing, wametembelea mji wa  Urumchi ambao ni mji mkuu wa mkoa huo wa Xinjiang wenye mamlaka ya ndani.

Keshavarz-Zadeh ameongeza kuwa, mji wa Urumchi ni mji maridadi sana na uliostawi na ambao una nembo kadhaa zenye kuashiria nukta za pamoja za utamaduni wa Iran na China. Amesema mji huu unakumbusha kuhusu zama za kunawiri mabadilishano ya kiutamaduni katika Barabara ya Hariri.

 Balozi Mohammad Keshavarz-Zadeh ameambatanisha ujumbe wake huo katika Twitter na picha kadhaa za safari yake mjini Urumchi.

Katika wiki za hivi karibuni Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya zimekuwa zikidai kuwa haki za jamii ya Uighur zinakiukwa katika mkoa Xinjiang na kwa msingi huo zimeiwekea China vikwazo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Hua Chunying hivi karibuni alitangaza katika mkutano na waandishi habari kuwa, kadhia ya Uighur si kadhia ya kikaumu, kidini au haki za binadamu bali ni kadhia ya kupambana na watu wanaotumia mabavu na wanaotaka kujitenga na China. Amesema Marekani haiwajali hata kidogo watu wa jamii ya Uighur bali kile inachokifuatilia ni kudhoofisha usalama na uthabiti wa China ili kwa njia hiyo kasi ya ustawi wa China ipungue.

 

 

3961825

captcha