IQNA

Mohammad Javad Zarif

Imam Khomeini (MA) alionyesha kuwa, kwa kuwategemea wananchi inawezekana kuyashinda madola ya kibeberu

19:51 - June 02, 2021
Habari ID: 3473972
TEHRAN (IQNA)- Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema pamoja na kuwepo kila aina ya njama za madola makubwa ya kibeberu, wananchi wa Iran leo wanasimama kidete na kwa heshima.

Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameyasema hayo Jumatano mjini Tehran alipohutubu katika Kongamano la Kimataifa la Fikra za Siasa kwa Mtazamo wa Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu Amrehemu). Zarif ameashiria kuhusu nafasi ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika mabadiliko ya mfumo wa kimataifa na kusema: "Kilichobainika wazi katika Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na fikra za Imam Khomeini (MA) ni kuwa, uwezo wa kimaada si nguzo pekee inayoibua nguvu duniani bali kuwategemea wananchi na irada yao pia kunaweza kuwa na nafasi yenye kuanisha hatima katika mfumo wa kimataifa."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema madola ya Magharibi na Mashariki katu hayakutaka Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yapate ushindi. Ameongeza kuwa, Imam Khomeini (MA) alionyesha wazi kuwa, kwa kuwategemea wananchi inawezekana kuyashinda madola makubwa ya kibeberu na kujiainishia mustakabali kinyume na yatakavyo madola hayo makubwa.

Zarif aidha amesema ingawa madola makubwa ya kibeberu ambayo yanategemea uwezo wao wa kifedha, yanaweza kuzishinikiza nchi zingine lakini hayawezi kudhibiti kikamilifu hatima na hali ya dunia. Amesema Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yameonyesha wazi kuwa, kwa kutegemea wananchi na kuwa na Imani kuhusu nguvu ya juu zaidi ya Mwenyezi Mungu SWT, inawezekana kusambaratisha njama za madola hayo ya kibeberu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekumbusha kuhusu njama za maadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na watu wa Iran na kusema, katika kipindi cha miongo minne iliyopita, Iran imekabiliwa na changamoto nyingi kama vile vita vya kulazimishwa vya utawala wa Baath wa Iraq dhidi ya Iran, vikwazo vya kiuchumi, vita vya kiuchumi, aina mbali mbali za ugaidi ukiwemo ugaidi wa kiuchumi, ugaidi wa kijeshi, ugaidi wa kimazingira, na ugaidi wa kimatibabu lakini leo pamoja na kuwepo mashinikizo hayo yote taifa la Iran linasimama kidete na kwa heshima.

Zarif ameashiria pia jibu kali la wanamapambano wa Palestina wakati wa kukabiliana na hujuma ya hivi karibuni ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Ukanda wa Ghaza na kusema: "Kile ambacho kimepelekea kufeli ngao ya makombora ya 'Kuba la Chuma' ya utawala wa Kizayuni ni imani imara ya Wapalestina kuhusu uwezo wao na  haki yao katika kujihami mkabala wa sera za kibaguzi na kiapathaidi za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Katika kukaribia mwaka wa 32 tokea aage dunia Imam Khomeini (MA), Kongamano la Kimataifa la Fikra za Siasa kwa Mtazamo wa Imam Khomeini (MA). Kongamano hilo ambalo lilikuwa na washiriki wengine wa kimataifa kwa njia ya intaneti pia limehutubiwa na mjukuu wa Imam Khomeini (MA), Hassan Khomeini. Kongamano hilo limefanyika katika Haram ya Imam Khomeini MA hapa nchini Tehran. 

3975322

Kishikizo: zarif ، iran ، Imam Khomeini
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
* :