Araghchi aliyasema haya katika hafla maalumu iliyofanyika asubuhi ya Jumamosi katika kaburi au haram tukufu ya Imam Khomeini (RA), kusini mwa Tehran, ambapo maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje walihuisha tena ahadi yao kwa misingi na malengo ya muasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Akitilia mkazo nafasi ya kipekee ya Imam Khomeini katika kupambana na uingiliaji wa mataifa ya kigeni, Araghchi amesema kwamba kupinga kwake mkataba wa utawala wa kibeberu (capitulation) kulianza taasisi iliyoimarisha kanuni ya “kupinga ubeberu” kama msingi madhubuti wa siasa ya nje ya Iran ya Kiislamu.
Amebainisha kuwa sera ya “Si Mashariki, wala Magharibi” , ambayo maana yake si kupinga uhusiano na mataifa hayo, bali ni kupinga kutawaliwa na kambi hizo mbili imetokana moja kwa moja na msingi huu wa kifikra.
Katika Katiba ya Iran, ibara ya pili inasema wazi kuwa Jamhuri ya Kiislamu ni mfumo uliojengwa juu ya msingi wa kukanusha dhulma, uonevu, kulazimisha au kukubali utawala wa kigeni.
“Huu ndio msingi wa mwenendo wetu wa kidiplomasia, na utaendelea kuwa hivyo,” amesisitiza Araghchi.
“Tumejitolea kama askari wa Imam Khomeini (RA) na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, na tunaomba kwa Mwenyezi Mungu tuwe askari wa kutegemewa,” akaongeza.
Kila mwaka, katika kipindi hiki, huandaliwa hafla ya kumbukumbu katika kaburi la Imam Khomeini kusini mwa Tehran, ambapo maelfu ya waombolezaji hushiriki. Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, hutoa hotuba katika tukio hauli hiyo kila mwaka.
Ayatullah Ruhullah Mousavi Khomeini, maarufu zaidi kama Imam Khomeini, ndiye aliyeongoza Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979 nchini Iran ambayo yaliuangusha utawala wa Mfalme (Shah) aliyekuwa kibaraka ya Marekani.
Imam Khomeini alizaliwa mwaka 1902, na baadaye akawa kiongozi mashuhuri wa harakati za watu wa Iran katika miaka ya 1970 dhidi ya mfumo wa kifalme wa karne nyingi.
Imam Khomeini aliaga dunia na kurejea kwa Mola wake tarehe 3 Juni, mwaka 1989 akiwa na umri wa miaka 87.
3493284