IQNA

Waziri Mkuu wa Iraq apongeza Harakati ya al Hashd al Shaabi kwa kuangamiza magaidi

21:53 - June 28, 2021
Habari ID: 3474050
TEHRAN (IQNA)- Harakati ya wapiganaji wa kujitolea wa wananchi wa Iraq maarufu kama Al Hashd al Shaabi (PMU) imefanya gwaride kubwa lililopewa jina la 'Idi ya Hashd' siku ya Jumamosi 26 Juni kwa mnasaba wa mwaka wa saba wa kuanzishwa kwake.

Harakati ya Al Hashd al Shaabi  iliundwa Juni 2014 kufuatia fatwa ya marjaa wa Iraq Ayatullah Sistani. Lengo la kuundwa harakati hiyo lilikuwa ni kupambana na kundi la kigaidi la ISIS au Daesh na kulinda mamlaka ya kujitawala Iraq. Kwa hivyo Al Hashd al Shaabi iliundwa kwa misingi ya kidini na kitaifa. Al Hashd al Shaabi  ilikuwa na nafasi muhimu sana katika kukabiliana na magaidi wa ISIS  nchini Iraq. Ni kwa kuzingatia nukta hiyo ndio  wakati alipokuwa waziri mkuu wa Iraq, Haidar al Ebadi mnamo 24 Februari 2016, wakati wa kukaribia kumalizika vita dhidi ya ISIS, alitoa amri kuwa Al Hashd al Shaabi ni taasisi ya kujitegemea ambayo itakuwa ikiendesha shughuli zake chini ya kamandi ya Majeshi ya Iraq.

Makundi ya kisiasa ya Iraq yanayounga mkono Al Hashd al Shaabi nayo pia mnamo 26 Novemba 2016 yaliunga mkono muundo mpya wa kijeshi wa kundi hilo kwa mujibu wa sheria za Iraq na kupelekea kupitishwa "Sheria ya Al Hashd al Shaabi " katika Bunge la Iraq. Baada ya kupitishwa sheria hiyo, Al Hashd al Shaabi  ilitambuliwa kama taaisi rasmi ya kiusalama na wanachama wake wakawa wanapata bajeti maalumu ya serikali.

Pamoja na kuwa Al Hashd al Shaabi ni kikosi rasmi cha kijeshi cha Iraq lakini kundi hilo limekuwa likipingwa na baadhi ndani na nje ya Iraq. Sababu kuu ya kupingwa Al Hashd al Shaabi  na baadhi ya watu ni kuwa ina fikra za kimuqawama au za mapambano ya Kiislamu na inapinga wazi wazi uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya Iraq. Aidha Al Hashd al Shaabi  inaamini kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel ndio chanzo kikuu cha ukosefu wa usalama katika eneo la Asia Magharibi. Hali kadhalika Al Hashd al Shaabi iko karibu na makundi mengine ya mapambano ya Kiislamu katika eneo. Kwa kuzingatia nukta hizo, gwaride kubwa la kijeshi  la Al Hashd al Shaabi lina umuhimu mkubwa na linaweza kuangaziwa kwa mitazamo kadhaa.

Kwanza kabisa, gwaride hilo limeweka wazi uwezo wake wa kijeshi na kivita. Gwaride hili limefanyika kama magwaride ya majeshi mengine makubwa duniani na hivyo limeweza kuonyesha wazi utayarifu wake mkubwa wa kivita. Kuhusiana na nukta hii, mkurugenzi wa habari katika Al Hashd al Shaabi, Mohanad Najim Aleqabi  amesema: "Mipangilio na uwezo wa kivita na kijeshi ni ujumbe muhimu zaidi wa gwaride la  al-Hashd al-Shaabi." Amesema harakati hiyo sasa ina nguvu zaidi ya ilivyokuwa katika miaka ya nyuma na sasa ni sehemu ya vikosi vya usalama vya Iraq.

Ujumbe mwingine  ni kuhudhuria gwaride hilo Waziri Mkuu wa Iraq Mustafa al Kadhimi akiwa ameandamana na waziri wa ulinzi. Akihutubu katika mjumuiko huo wa kijeshi al Kadhimi alisema al-Hashd al-Shaabi ilifanikiwa kuangamiza magaidi wakufurushaji wa ISIS. Hivyo waziri mkuu wa Iraq amekiri kadamnasi kuhusu uwezo mkubwa wa al-Hashd al-Shaabi. Ujumbe mwingine ni kuwa wapinzani walifeli kumzuia Al Kadhimi kuhudhuria na kuhutubu katika gwaride hilo kiasi kwamba liliakhirishwa kwa siku 13. Wapinzani wa kundi hilo waliamini kuwa kuhudhuria Al Kadhimi katika gwaride hilo kungelipa itibari muhimu kundi la  al-Hashd al-Shaabi na hivyo kufelisha mbinu na njama za kuliharibia jina.

Ujumbe mwingine wa gwaride hilo ni kuwa kinyume na propaganda za wapinzani, al-Hashd al-Shaabi ni kundi lisilofungamana na kabila, kaumu, dini au madhehebu kwani katika gwaride hilo ilibainika wazi kuwa wanachama wake ni kutoka maeneo yote ya Iraq wakiwemo Waislamu wa madhehebu ya Shia na Suni na Wakristo.

Kwa kuzingatia nukta hizo muhimu, wapinzani wa al-Hashd al-Shaabi wamekuwa wakifanya kila wawezalo kuligonganisha kundi hili na Jeshi la Iraq lakini bila mafanikio.

3980062

captcha