IQNA

Maziko ya wapiganaji wa al Hashdi Shabi ya Iraq waliouawa na Marekani

22:43 - June 29, 2021
Habari ID: 3474054
TEHRAN (IQNA)- Mazishi ya wanachama wanne wa Harakati ya wapiganaji wa kujitolea wa wananchi wa Iraq maarufu kama Al Hashd al Shaabi (PMU) ambao wameuawa na Marekani yamefanyika leo Baghdad, Iraq.

Wapiganaji hao wa al Hashd al Shaabi waliuawa shahidi wakati jeshi dhalim la Marekani liliposhambulia wapiganaji wa harakati za Kiislamu katika mpaka wa Iraq na Syria hivi karibini.

Walioshiriki katika maziko hayo wametoa nara dhidi ya Marekani na utawala haramu wa Israel.

Wakati huo huo, Makundi ya muqawama ya Iraq yametangaza kuwa, yatalipiza kisasi mashambulizi ya Marekani dhidi ya ngome za kundi la Hashdu Shaabi.

Makundi ya muqawama ya Iraq jana Jumatatu yalitoa taarifa ya pamoja katika radiamali yao kwa mashambulizi ya Marekani dhidi ya ngome za Hashdu Shaabi katika mpaka wa Syria na Iraq na kueleza kuwa: 'Sisi hatutakaa kimya mkabala na kuendelea kuwepo wanajeshi vamizi wa Marekani nchini; hatua inayokinzana na katiba, uamuzi wa bunge na matakwa ya wananchi wa Iraq.'

Makundi ya muqawama ya Iraq yamesema kuwa, vikosi vamizi vya Marekani vingali vinaendeleza jinai zao huko Iraq kwa kuwashambulia wanamuqawama wa harakati ya Hashdu Shaabi na kusisitiza kuwa, watalipiza kisasi cha damu za mashahidi wa mashambulizi hayo na kuwa adui ataonja ladha chungu ya kisasi hicho.  

Kundi la muqawama la Kataeb Sayyid Shuhada la Iraq pia awali lilitangaza kuwa, kuanzia sasa vita baina yao na wanajeshi vamizi wa Marekani havitakuwa na mipaka; na kwamba hatua ya kwanza ya vita hivyo ni kuzishambulia ndege za wanajeshi hao vamizi katika anga ya Iraq. 

Vyombo vya habari  huko Iraq na Syria jana asubuhi vilitangaza habari ya kujiri mashambulizi ya anga ya marekani katika ngome za kundi la Hashdu Shaabi katika eneo la Bukamal katika mpaka wa Syria na Iraq. Wanamuqawama wanne wa Hashdu Shaabi wameuliwa shahidi na watatu wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo. 

/3475098

captcha