IQNA

Hafla za "Watoto Wanaonyonya wa Hussein" zafanyika kimataifa

TEHRAN (IQNA)- Hafla za Kimataifa kwa jina la "Watoto Wachanga Wanaonyonya wa Hussein AS" zimefanyika leo Ijumaa katika maeneo mbalimbali hapa nchini Iran na katika nchi 45 duniani sambamba na Ijumaa ya kwanza ya mwezi wa Muharram.

Hafla hizo za kimataifa za Watoto Wachanga Wanaonyonya wa Hussein AS ni mjumuiko wa kidini unaofanywa na Waislamu duniani ikiwemo hapa Iran, India, Pakistan, Iraq, Saudia, Uturuki na Afghanistan katika Ijumaa ya kwanza ya mwezi wa Muharram katika kuwakumbuka watoto waliouliwa shahidi katika Siku ya Ashura.

Katika marasimu haya, akina mama huwavalisha watoto wao wachanga mavazi yenye kufanana na kisha huwafunga vipande vya vitambaa kichwani vilivyoandikwa jina tukufu la Ali Asghar a.s.; na hivyo kudhihirisha mapenzi na kujitolea kwao kwa familia  hiyo tukufu. 

Mtukufu Ali Asghar AS alikuwa mtoto mdogo zaidi wa Imam Hussein AS; Imamu wa tatu wa Waislamu wa Kishia ambaye aliuliwa shahidi tarehe Sita Muharram mwaka 61 Hijria huko Karbala  akiwa na umri wa miezi sita.

Itakumbukwa kuwa tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijria yaani miaka 1382 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, moja kati ya vita mashuhuri katika historia ya Kiislamu na ya mwanadamu, vilitokea baina ya majeshi ya haki na batili katika ardhi ya Karbala huko Iraq.

Siku hii inajulikana kwa jina la Ashura. Katika siku hiyo mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS, alisimama kishujaa na wafuasi wake waaminifu 72, kukabiliana na jeshi la batili la Yazid bin Muawiya ili kuilinda dini ya Allah na hatimaye waliuawa Shahidi.

3990389