IQNA

Marufuku ya maombolezo ya Muharram yaripotiwa tena nchini Bahrain

15:08 - July 13, 2025
Habari ID: 3480936
IQNA – Kama ilivyokuwa katika miaka iliyopita, mamlaka za Bahrain zimeendelea kuweka vizuizi juu ya maombolezo ya Muharram, hasa katika siku ya Ashura, mwaka huu pia.

Dua kwa ajili ya mashujaa wa Ummah wa Kiislamu zilipigwa marufuku, huku wahubiri na wasomaji wa mashairi ya maombolezo wakilengwa kwa bughudha na usumbufu.

Kama kila mwaka, mwezi wa Muharram , hasa siku ya Ashura , umekuwa wakati wa mashinikizo ya kisekta na kisiasa dhidi ya Waislamu wa Kishia nchini Bahrain.

Hali hii imejitokeza kupitia vitendo vya maafisa wa serikali kuondoa bendera nyeusi na mahema ya maombolezo, pamoja na maafisa wa usalama waliovaa mavazi ya maafisa wa manispaa wakidai kuwa ni kwa ajili ya “mpangilio,” ilhali nia ni kuzuia ibada na shughuli za maombolezo ya Muharram.

Hatua hizi zilielezewa zaidi katika onyo lililotolewa na Rashid Al Khalifa, waziri wa mambo ya ndani wa Bahrain, katika kikao na viongozi wa vituo vya maombolezo na kumbi za kidini zijulikanazo kama Husseiniya, ambapo alidai kuwa maombolezo ya Muharram ni mwanya wa Waislamu wa Kishia kufanya mikutano ya kisiasa na kueneza vurugu dhidi ya utawala wa kifalme wa Al Khalifa.

Sheikh Ibrahim al-Aradi, mkuu wa idara ya kisiasa ya Muungano wa Februari 14, alisema kuwa, “Mkutano wa kila mwaka ulioitishwa na waziri wa mambo ya ndani mwaka huu ulikuwa wa kipekee kwa ujumbe aliotuma hata nje ya mipaka ya Bahrain. Alijaribu kuishambulia Iran kwa kudai kuwa Ashura ilikuwapo Bahrain kabla hata ya Iran, lakini alikosea, kwa sababu Ashura ilikuwa Bahrain hata kabla ya utawala wa Al Khalifa.”

Alisisitiza kuwa simulizi inayosambazwa na vyombo vya habari rasmi kuwa serikali inalinda mwezi wa Muharram na siku ya Ashura si ya kweli bali ni kinyume chake.

Kiongozi huyo wa Muungano wa Februari 14 alibainisha kuwa mashambulizi dhidi ya Waislamu wa Kishia yamekuwepo kwa muda mrefu, lakini hukithiri zaidi katika mwezi wa Muharram, kwa sura mbalimbali.

Jambo hili liliongezeka zaidi baada ya harakati za kupinga utawala mnamo Februari 2011. Katika wiki ya kwanza tu ya Muharram mwaka huu, zaidi ya wahubiri 15 waliitwa na maafisa wa usalama, na baadhi yao kukamatwa.

Katika baadhi ya maeneo, maafisa wa usalama walifika na hata kupiga marufuku uvaaji wa vitambaa vya kichwani vyenye maneno ya Husseini na mashati yaliyoonyesha maombolezo ya kidini.

349380

Kishikizo: bahrain ashura muharram
captcha