IQNA

Kamera 2,000 za usalama zatazama shughuli za maombolezo Karbala

14:14 - June 23, 2026
Habari ID: 3482392
IQNA – Katika jitihada za kuimarisha usalama na kuhakikisha utulivu wakati wa siku tukufu za Tasua na Ashura katika mji mtakatifu wa Karbala, nchini Iraq, jumla ya kamera 2,000 za kisasa (smart cameras) zimewekwa kama sehemu ya mpango maalum wa kiusalama.

Idara ya Mawasiliano na Usalama wa Habari ya Astan (Uongozi) katika Haram Tukufu ya Hadhrat Abbas (AS) imetangaza hatua hiyo, ikibainisha kuwa lengo kuu ni kusimamia mikusanyiko mikubwa, kuhakikisha usalama wa mazuwari, na kufuatilia kwa karibu maombolezo ya kijadi ya Rakdha Tuwairaj katika wakati halisi (real-time), kwa mujibu wa ripoti ya Al-Kafeel.

Idara hiyo imeeleza kuwa, ndani ya mfumo wa mipango ya kiusalama na huduma kwa ajili ya siku ya 10 ya Muharram huko Karbala na maombolezo ya Rakdha Tuwairaj, kamera hizo takriban 2,000 zimesambazwa katika maeneo mbalimbali ya mji huo.

Mhandisi Muhammad Raad Al-Asfour, afisa katika idara hiyo, alisema kuwa timu za kiufundi zimeanza maandalizi hayo kwa muda mrefu ili kuwapokea mazuwari wa Imam Hussein (AS) na Hadhrat Abbas (AS) kwa heshima na usalama.

Alibainisha kuwa hatua hizo zinahusisha kuimarisha miundombinu ya mfumo wa ufuatiliaji, ukaguzi wa kiufundi, na matengenezo ya kamera zilizopo ndani na nje ya Haram Tukufu, pamoja na mitaa na maeneo yanayozunguka mji huo.

“Lengo la hatua hizi ni kufuatilia hali ya msongamano wa watu wakati wa shughuli za Ashura na Rakdha Tuwairaj ili, endapo kutatokea msongamano mkubwa au hali yoyote ya dharura, taasisi zinazohusika ziweze kuchukua hatua za haraka na kuelekeza umati ipasavyo,” alisema.

Akizungumzia ukubwa wa mfumo huo wa ufuatiliaji, Al-Asfour alifafanua kuwa mtandao huo unajumuisha kamera 2,000 za kudumu na zinazohamishika zilizowekwa katika mji wa kale wa Karbala na viunga vyake.

Aliongeza kuwa kamera za kisasa za kutambua nyuso (facial recognition), za kuhesabu mazuwari, na kamera za kunasa joto (thermal cameras) pia zimejumuishwa katika mradi huo.

Alisisitiza kuwa vifaa vyote hivi vinatumia mifumo ya kisasa inayowezeshwa na teknolojia ya akili mnemba (AI) na vitachukua nafasi kubwa katika kuimarisha usalama, kusimamia makundi ya watu, na kurahisisha utoaji wa huduma kwa mazuwari.

Hatua hizi ni sehemu ya mpango mpana wa kiusalama na kijamii wa Astan ili kuhakikisha kuwa maombolezo ya Ashura yanafanyika kwa utukufu mkubwa, amani, na utulivu.

/3497941

captcha