IQNA

Maombolezo kwa mnasaba wa Tasu'a katika mwezi wa Muharram

11:09 - August 18, 2021
Habari ID: 3474202
Katika mkesha Tasu'a ya Imam Hussein AS, waislamu, hasa wa Madhehebu ya Shia wameghiriki katika maombolezo kwa mnasaba wa siku hii.

Leo Jumatano ni tarehe 9 Muharram mwaka 1443 Hijria Qamaria sawa na 18 Agosti 2021 na siku hii ni maarufu kama Tasu'a ya Imam Hussein AS, Imamu wa Tatu wa Waislamu wa Madhehebu ya Shia ambaye aliuawa shahidi akiwa na wafuasi wake watiifu akiwemo ndugu yake,  Abul Fadhl Abbas AS.

Kwa mnasaba wa kumbukumbu ya yaliyojiri siku ya Tasu'a, kote katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kumeshuhudiwa mijumuiko ya maombolezo.

Katika siku kama hii mwaka 61 Hijria wakati majeshi ya Yazid yalikuwa yamejiandaa kikamilifu kumshambulia Imam Hussein AS na masahaba zake katika ardhi ya Karbala, Imam alimtuma ndugu yake aliyesifika kwa ushujaa mkubwa yaani Abul Fadhl Abbas AS akawaombe maadui hao wampe fursa aupitishe usiku huo, kwa Swala na kunong'ona na Mola wake. Kwa msingi huo siku hii hukumbukwa kama siku ya ushujaa na ujasiri wa Abul Fadhl Abbas AS. Abul Fadhl al Abbas aliuawa shahidi baada ya kukatwa mikono yote miwili na maadui wa Watu wa Nyumba ya Mtume wetu Muhammad SAW wakiongozwa na Yazid bin Muawiyah.

Watu 72 waliokuwa katika kambi ya Imam Hussein AS huko Karbala wote waliuawa shahidi  tarehe 10 Muharram yaani Siku ya Ashura, wakiwa pamoja na kiongozi wao katika mapambano ya haki dhidi ya dhulma na uonevu na hivyo wakaweza kuunusuru Uislamu.

Mwaka huu kutokana na janga la COVID-19 vikao vya maombolezo havikufanyika ndani ya misikiti au ndani ya kumbi bali zimefanyika katika maeneo ya wazi ambapo waombolezaji wamezingatia kanuni za kiafya katika kipindi hiki.

3991495/

captcha