IQNA

Mtazamo kuhusu hali ya mambo nchini Afghanistan

23:51 - August 28, 2021
Habari ID: 3474235
TEHRAN (IQNA)- Matukio ya majuma mawili ya hivi karibuni nchini Afghanistan yameonyesha kuwa, makundi ya mapambano na muqawama katika eneo la Asia Magharibi yana nafasi muhimu katika kulinda mamlaka ya kujitawala pamoja na usalama wa mataifa yao.

Katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, Afghanistan ilishuhudia matukio mawili muhimu. Awali tarehe 15 Agosti wanamgambo wa Taliban waliingia katika mji mkuu wa nchi hiyo Kabul na kuchukua madaraka ya nchi baada ya Rais Muhammad Ashraf Ghani kuikimbia nchi. Wanamgambo wa Taliban walichukua udhibiti na hatamu za uongozi wa nchi bila ya upinzani wowote, na tena katika kipindi kifupi tu. Hali hiyo imewafanya wananchi wa nchi hiyo hususan wa mji mkuu Kabul kuanza kuikimbia nchi. Wananchi wa Afghanistan wamekuwa wakiikimbia nchi wakitumia mipaka ya ardhini na kukusanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kabul wakiwa na nia ya kuondoka nchini humo. Woga walionao kwa kundi la Taliban inatajwa kuwa sababu kuu ya wananchi wa Afghanistan kutaka kuikimbia nchi. Hata hivyo, kukusanyika wananchi katika Uwanja wa Ndege wa Kabul kumeongeza hatari ya kufanyika shambulio la kigaidi, ambapo Alkhamisi ya juzi tarehe 26 Agosti kwa akali watu 200  waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika shambulio la kujilipua jirani na Uwanja wa Ndege wa Kabul. Kundi la kigaidi la ISIS au Daesh Ukanda wa Khorassan (ISIS-K) limetangaza kuhusika na hujuma hiyo ambayo ni ya kwanza kutokea mjini Kabul tangu rais Ashraf Ghani aitoroke nchi; na mji mkuu huo wa Afghanistan kudhibitiwa na kundi la Taliban mnamo tarehe 15 Agosti.

Nchi isiyo na jeshi

Kwa hakika matukio ya Afghanistan yameonyesha kuwa, kivitendo nchi hiyo haina jeshi na wananchi hawana ulinzi. Kuangukia mji wa Kabul mikononi mwa Taliban katika kipindi cha muda mfupi, kabla ya kila kitu kumeonyesha kwamba, uwepo wa makundi ya muqawama katika baadhi ya nchi za Kiarabu katika eneo, ni jambo muhimu la kistratejia na linalodhamini mamlaka ya kujitawala, usalama na umoja wa ardhi yote ya mataifa hayo.

Harakati za muqawama au mapambano ya Kiislamu nchini Syria, Iraq, Yemen, Lebanon na Palestina zinaoneysha kuwa , muqawama katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) ni mkakati muhimu kwa mataifa ambayo ndani yake kuna makundi ya muqawama. Makundi ya muqawama siyo tu kwamba, yamejiimarisha kijeshi bali moyo wa muqawama umeimarika na kupata nguvu baina ya wananchi na waungaji mkono wake, kiasi kwamba, hii leo hakuna mtu anayezungumzia suala la kuangushwa tawala za Syria, Iraq, Yemen na Lebanon au Palestina katika Ukanda wa Gaza. Fawzi Barhoum, msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina anasema kuhusiana na hili kwamba, kama kusingekuweko muqawama na wananchi wa Palestina, basi leo malengo ya Wapalestina yangekuwa yamekwishasahaulika.

Hapana shaka kuwa, matukio ya Afghanistan kabla ya kila kitu, yameonyesha kuwa, muqawama ni kitu kilichopotea katika nchi hiyo, na kuiamini Marekani ulikuwa mkakati mbaya na usio sahihi wa watawala wa zamani wa Afghanistan.

3993322

captcha