IQNA

Watoto 33,000 wauawa, walemazwa wakati wa uvamizi wa Marekani Afghanistan

19:40 - September 01, 2021
Habari ID: 3474248
TEHRAN (IQNA)- Karibu watoto 33,000 wameuawa na kulemazwa nchini Afghanistan katika kipindi cha miaka 20 iliyopita wakati wa uvamizi wa Marekani dhidi ya nchi hiyo, limesema shirika la Save the Children.

Katika taarifa iliyotolewa baada ya askari wa mwishi wa Marekani Jumatatu, shirika la misaada limesema idadi hiyo inaashiria nanma uvamizi wa Marekani Afghansitan ulivyosababisha maafa kwa watoto katika nchi hiyo.

Halikadhalika  Save the Children imesema idadi halisi ya watoto waliouawa moja kwa moja kwenye mzozo huo yamkini ni zaidi ya  iliyokadiriwa ambayo pia haijumuishi watoto ambao wamekufa kwa sababu ya njaa, umaskini na magonjwa kutokana na uvamizi wa Marekani.

Hata kabla ya kuongezeka kwa vurugu hivi karibuni, karibu nusu ya idadi ya watu wa Afghanistan - pamoja na watoto karibu milioni kumi - walikuwa wakihitaji msaada wa kibinadamu kutokana ukame, wimbi la tatu la COVID-19 na vile vile mgogoro wa muda mrefu. Nusu ya watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano wanakabiliana na utapiamlo mkali mwaka huu.

"Wakati ndege za mwisho za kijeshi zikiruka kutoka Kabul leo ni ukweli wa kusikitisha kwamba, pamoja na ndege,  uzingatiwaji wa  kimataifa,  na msaada ambayo Afghanistan imepokea katika wiki chache zilizopita pia ina uwezekano wa kuondoka. Mamilioni ya watoto wa Afghanistan watalala usiku huu wakiwa na njaa, wakiwa na huzuni na hawajui nini hatima yao, "Mkurugenzi wa Kikanda cha Asia wa Save the Children Hassan Noor alisema.

Wito wa Umoja wa Mataifa

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuwa, Afghanistan inakaribia kutumbukia katika janga la kibinadamu.

Antonio Guterres, sambamba na kuashiria kushtadi mgogoro wa kibinadamu na kiuchumi na kusambaratika sekta ya utoaji huduma nchini Afghanistan amesema kuwa, hali inavyoonekana ni kuwa, nchi hiyo inaelekea kukumbwa na maafa ya kibinadamu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, hivi sasa nusu ya wananchi wa Afghanistan wanahitajia misaada ya kibinadamu ili waweze kuendelea kuishi.

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa inaeleza kuwa,  hivi sasa wanaume, wanawake na watoto wa Afghanistan wanategemea zaidi misaada ya jamii ya kimataifa kuliko wakati mwingine wowote ule.

Jumapili tarehe 15 mwezi uliopita wa Agosti serikali ya Rais Muhammad Ashraf Ghani ilisambaratika na kiongozi huyo kuikimbia nchi baada ya Taliban kuingia Kabul mji mkuu wa Afghanistan. Wachambuzi wa mambo wanasema, hatua ya wanamgambo wa Taliban ya kuudhibiti mji wa Kabul imehitimisha uvamizi wa miaka 20 wa Marekani na nchi nyingine za Magharibi kwa kisingizio cha kuijenga upya Afghanistan.  Aghalabu ya viongozi na wananchi wa Afghanistan wanaamini kuwa, hali ya sasa ya nchi hiyo ni matokeo ya siasa zilizofeli za Marekani nchini humo.

3475601

Kishikizo: afghanistan watoto
captcha