IQNA

Iran yalaani hujuma ya kigaidi mjini Kabul, Afghanistan

14:13 - August 27, 2021
Habari ID: 3474230
TEHRAN (IQNA)- Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali mashambulio ya kigaidi yaliyotokea katika eneo la uwanja wa ndege wa Kabul nchini Afghanistan jana Alkhamisi.

Katika taarifa Saeed Khatibzadeh Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametoa salamu za rambirambi za serikali na watu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa taifa la Afghanistan na kuwaombea rehma na maghufira ya Mwenyezi Mungu walioaga dunia katika hujuma hiyo ya kigaidi, sanjari na kuwatakia shifaa ya haraka majeruhi wa mashambulizi hayo.

Amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesikitishwa sana na kuuliwa bila ya hatia raia wa kawaida katika mashambulio hayo ya Kabul, wakiwemo wanawake, watoto na vijana.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amebainisha kuwa: Tunatumai serikali jumuisha itaundwa huko Kabul haraka iwezekanavyo, ili mamlaka husika zichukue jukumu la kulinda maisha na mali za Waafghani.

Watu 110 raia wa Afghanistan wametihibitishwa kuuawa katika hujuma hiyo ambayo pia ilipelekea askari 13 wa Jeshi la Marekani kuangamizwa. Kundi la Taliban ambalo linashikilia madaraka Afghanistan limesema Jeshi la Marekani ndilo lililokuwa na jukumu la kudumisha usalama katika eneo la hujuma hiyo ya kigaidi.

Wakati huohuo, kundi la kigaidi la ISIS au Daesh Ukanda wa Khorassan (ISIS-K) limetangaza kuhusika na hujuma hiyo ambayo ni ya kwanza kutokea mjini Kabul tangu rais Ashraf Ghani aitoroke nchi; na mji mkuu huo wa Afghanistan kudhibitiwa na kundi la Taliban mnamo tarehe 15 Agosti.

Kupitia shirika lake la habari za kipropaganda la Amaq, genge hilo la kigaidi na kitakfiri limetangaza kuhusika na miripuko hiyo ya jana.

Taarifa ya ISIS iliyotumwa kwenye ukurasa wake wa Telegram imesema: Mwanachama wa Daesh aliyekuwa amejifunga mabomu alifanikiwa kupenya na kuufikia ummati mkubwa wa wakalimani na washiriki wa jeshi la Marekani katika kambi ya Baran karibu na Uwanja wa Ndege wa Kabul na kujiripua.

Kabla ya ISIS kutoa tamko hilo, maafisa wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon walisema, wanaitakidi kuwa kundi la kigaidi la ISIS ya Khorasan ndilo lililohusika na miripuko hiyo ya jana iliyotokea katika mazingira ya mtafaruku na msongamano wa watu waliomiminika katika uwanja wa ndege wa Kabul kwa lengo la kuihama nchi.

Wakati huohuo, Rais Joe Biden amesema kamwe Marekani haitosahau wala kusamehe mashambulio hayo, na kwamba italipiza kisasi.

3203478

captcha