IQNA

Wasifu wa mwanakemia Muirani Muislamu wachapishwa Uganda

22:45 - August 29, 2021
Habari ID: 3474237
TEHRAN (IQNA)- Kituo cha Utamaduni cha Iran nchini Uganda kimesambaza katika mitandao ya kijamii wasifu wa mwanakemia Mwislamu Muirani Zakaria Razi.

Tarehe 26 Agosti ni siku aliyozaliwa Muhammad bin Zakaria Razi, msomi, tabibu na mkemia mkubwa wa Kiislamu na Kiirani katika karne ya tatu Hijria.

Ni kwa msingi huo ndio Kituo cha Utamaduni cha Iran mjini Kampala, Uganda kikaamua kuchapisha makala kuhusu msomi huyu ambaye ni fahari kwa Waislamu na dunia nzima kwa ujumla.

Razi alizaliwa katika mji wa Rei nchini Iran mwaka 251 Hijria sawa na mwaka 865 Miladia katika zama za utawala wa Wasamani na kipindi cha karne za kati barani Ulaya. Mji wa Rei una historia ya miaka mingi na ulikuwa na wakazi katika kipindi cha zaidi ya miaka elfu tatu kabla ya kuzaliwa Nabii Isa Masiih AS. Baba wa historia ya elimu, George Sarton, anasema: Muhammad Zakaria Razi alikuwa daktari mkubwa zaidi wa Kiislamu katika karne za kati. Naye mtaalamu wa historia ya elimu, Julius Ruska amesema: Razi ndiye baba wa elimu ya kemia na mwasisi wa mfumo mpya wa sayansi. 

Zakaria Razi alisifika sana kwa uhodari na uwezo wake mkubwa wa kihifadhi na kushika mambo mengi kichwani mwake. Ameandika katika kitabu chake alichokipa jina la "Shaka Kuhusu Galinos" (Doubts About Galen) akisema: "Katika ujana wangu nilikuwa na hamu kubwa ya kufanya majaribio ya vitu mbalimbali". Ni hamu hii kubwa ya Razi ndiyo iliyomuelekeza katika elimu ya kemia na kugundua mada iliyobadili chuma cha kawaida na kukifanya chuma chenye thamani kubwa hususan dhahabu. Hata hivyo wakati anafanya kazi na majaribio ya mada za kemikali na karibu na moto, macho ya Razi yalipatwa na madhara. Hivyo aliamua kwenda kwa daktari kutibu macho yake. Gharama ya matibu yake wakati huo ilikuwa karibu dinari mia tano, ambazo zilikuwa fedha nyingi sana kipindi hicho. Wakati alipokuwa akilipa gharama za matibabu, Zakaria Razi alijisemeza mwenyewe kwamba: "Hii ndiyo kemia na si kazi unayoifanya wewe kwa sasa ewe Razi"!

Tangu wakati huo Muhammad Zakaria Razi aliacha elimu ya kemia na kuanza kusoma elimu ya utabibu. Alifanya jitihada kubwa kwa ajili ya kufikia muradi wake. Mtu mmoja aliyeishi na Razi mjini Rei anasema: "Siku zote alitembea na kalamu na karatasi na daima alionekana akiandika". 

Muhammad bin Zakaria Razi alipitisha kipindi cha mwishoni mwa umri wake katika mji wa Rei ambako alifundisha na kulea wanafunzi wengi waliotokea kuwa mabingwa katika elimu ya udaktari. Kipindi hicho macho ya Razi yaliingiwa na mtoto wa jicho na mmoja wa wanafunzi wake kutoka Tabaristan alikwenda Rei kwa ajili ya kumtibu mwalimu wake. Razi alimwambia mwanafunzi kwamba, kazi hiyo itamzidishia mashaka na maumivu na kwamba anahisi kifo chake kilikuwa kimekaribia; hivyo hakuna haja ya kujitia mashakani kwa ajili ya kurejesha uwezo wake wa kuona.

/3993785/

Kishikizo: zakaria razi uganda
captcha