IQNA

Katika mahojiano ya kwanza tokea aachiliwe huru

Sheikh Zakzaky: Waliowengi Nigeria wanaunga mkono mfumo wa Kiislamu

21:35 - September 29, 2021
Habari ID: 3474360
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria Sheikh Ibrahim Zakzaky amesema waliowengi nchini humo wataunga mkono mfumo wa utawala wa Kiislamu iwapo watapewa hiari ya kuchagua.

Katika mahojiano maalumu na televisheni ya Press TV ambayo ni ya kwanza tokea aachiliwe huru, Sheikh Zakzaky amesema: “Naamini kuwa, iwapo kutafanyika kura ya maoni katika nchi hii (Nigeria) na wananchi waulizwe ‘unataka mfumo upi wa utawala? Ni mfumo wa sasa ambao ni mirathi ya wakoloni Waingereza au ni mfumo wa Kiislamu?, nina uhakika waliowengi watauchagua mfumo wa Kiislamu kwa sababu mfumo huu utakuwa ni wa wananchi.”

Akihojiwa na mwandishi maarufu wa Press TV Bi. Marzieh Hashemi,Sheikh Zakzaky amesema ingawa watawala wa sasa wa Nigeria katu hawawezi kuafiki kura ya maoni kama hiyo, lakini hilo haliondoi uwezekano wa kuanzishwa mfumo wa Kiislamu Nigeria. Amesisitiza kuwa uanzishwaji mfumo kama huo utategemea wananchi kupewa fursa ya kuchagua kama ilivyofanyika wakati wa kura ya maoni baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ya mwaka 1979.

Halikadhalika amesema viongozi wa Nigeria wakiwa katika vikao vyao vya faragha wanakiri kuwa wanaiogopa harakati ya Kiislamu nchini humo kwani wanaamini kuwa yamkini ikachangia kuanzishwa mfumo wa Kiislamu kama ule wa ‘Mapinduzi ya Kiislamu’ ya Iran. Sheikh Zakzaky amesema kile ambacho Harakati ya Kiislamu ya Nigeria inataka ni demokrasia kwani demokrasia halisi inamaanisha utawala wa wananchi waliowengi.

Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria aidha amesisitiza kuwa, matembezi ya Arubaini ya Imam Husain AS yataendelea kufanyika nchini Nigeria hadi atakapodhihiri Imam wa Zama, Imam Mahdi AS.

Ameongeza kuwa, askari wa serikali ya Nigeria hawawezi kukwamisha matembezi hayo kwa kuwapiga kwao risasi Waislamu wanaoshiriki kwenye matembezi hayo. 

Mahojiano hayo yamefanyika katika hali ambayo jeshi la polisi la Nigeria siku ya Jumanne liliwashambulia Waislamu waliokuwa wanashiriki katika matembezi ya Arubaini ya Imam Husain AS na kuwaua shahidi Waislamu wanane.

Abdullah Muhammad, mwanachama mwandamizi wa harakati hiyo amesema, walioshiriki kwenye matembezi ya Arubaini ya Imam Husain AS walikuwa wanafanya matembezi hayo kwa njia ya amani bila ya kuhatarisha usalama wa mtu yeyote, lakini pamoja na hayo polisi waliwafyatulia risasi Waislamu hao na kuwaua shahidi wanane kati yao.

Sheikh Ibrahim Zakzaky na mke wake, Mallimah Zeenah walitiwa nguvuni tarehe 13 Disemba mwaka 2015 katika shambulizi lililofanywa na jeshi la Nigeria dhidi ya kituo cha kidini cha Baqiyyatullah katika mji wa Zaria na walikuwa mahabusu kwa kipindi chote cha miaka 6 iliyopita kabla ya kuachiliwa huru mwezi Julai mwaka huu.

Karibu wafuasi 1,000 wa harakati ya Kiislamu ya Nigeria waliuawa kwa umati na vikosi vya usalama katika shambulizi hilo.

4001326

captcha