IQNA

IHRC yalaani askari wa Nigeria kwa kuhujumu matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein AS

14:13 - September 30, 2021
Habari ID: 3474363
TEHRAN (IQNA)-Tume ya Kiislamu ya Haki za Binadamu (IHRC) imelaani vikali hujuma ya askari wa Nigeria dhidi ya matembezi ya amani ya Siku ya Arubaini ya Imam Hussein AS Jumanne katika mji mkuu wa nchi hiyo, Abuja.

Watu  8 hadi sasa wamethibitishwa kuuawa shahidi katika hujuma hiyo ya askari wa Nigeria, imesema taarifa hiyo ya IHRC.

Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, inayoongozwa na Sheikh Ibrahim Zakzaky, Jumanne usiku ilitangaza kuwa askari usalama wa nchi hiyo wamewafyatulia risasi waombolezaji waliokuwa wamekusanyika katika marasimu ya  arubaini ya Imam Hussein AS huko Abuja. Abdullah Muhammad mwakilishi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ameeleza kuwa, waombolezaji katika marasimu hayo ya arobaini walikuwa wakielekea kwa amani katika barabara ya Abuja -Kubwa wakati walipofyatuliwa risasi na polisi na kuongeza kuwa watu 8 wameuawa shahidi katika hujuma hiyo.

IHRC imesema ina picha na klipu za video zinazoonyesha namna polisi walivyowafyatulia risasi waumini katika maandamano hayo.

Maadhimisho siku ya Arubaini hufanyika kila mwaka tarehe 20 Safar, kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Qamaria, baada ya kupita siku Arubaini tangu tarehe 10 mwezi wa Muharram, kwa ajili ya kukumbuka siku aliyouawa shahidi mjukuu wa Mtume SAW, Imam Hussein AS na masahaba zake ambao walijitolea roho zao kwa ajili ya kuhuisha dini ya Mwenyezi Mungu katika jangwa la Karbala mwaka 61 Hijria Qamaria. Haram Takatifu ya Imam Hussein AS iko katika mji huo wa Karbala.

3475847

captcha