IQNA

Kiongozi Muadhamu ahudhuria kikao cha maombolezo ya kuuawa shahidi Imam Ridha AS

19:08 - October 07, 2021
Habari ID: 3474392
TEHRAN (IQNA)- Maombolezo ya kukumbuka mwaka alipouawa shahidi Imam Ali bin Musa al Ridha AS, Imam wa Nane wa Waislamu wa Kishia duniani yamefanyika katika Husainia ya Imam Khomeini MA hapa mjini Tehran na kuhudhuriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.

Akitoa hotuba fupi katika maombolezo hayo, Hujjatul Islam Walmuslimin Rafi'i amenukuu hadithi mbalimbali za maasumu kuhusu Imam Ridha AS na pia kutoka kwa mtukufu huyo na matarajio yake kwa wafuasi wa Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad SAW.

Katika sehemu moja ya hotuba yake amesema, hekima na busara katika mambo, istiqama yaani kutotetereka katika njia ya wilaya, kuwa na misimamo ya wastani ya kimantiki na kujiepusha na misimamo mikali na ya kuchupa mipaka, kuifanya Qur'ani Tukufu kuwa ndiyo marejeo makuu pamoja na sunna na sira za maasumu katika maisha ya kila mmoja wetu na ya kijamii, kuheshimu sheria na kila mmoja kutekeleza inavyopasa majukumu yake, ni miongoni mwa mambo ambayo Imam Ridha AS anayetarajia kutoka kwa wafuasi wa Ahlul Bayt wa Mtume SAW. 

Katika maombolezo hayo, malenga wa kusifu kizazi kitoharifu cha Bwana Mtume Muhammad SAW wamesoma mashairi mbalimbali ya kutaja masaibu yaliyokikumba kizazi hicho kitoharifu cha mtukufu wa daraja.

Ikumbukwe kuwa, leo Alkhamisi, tarehe 30 Mfunguo Tano Safar 1443 Hijria sawa na tarehe 7 Oktoba 2021 Milaadia, imesadifiana na maombolezo ya kukumbuka mwaka alipouawa shahidi Imam wa Nane wa Waislamu wa Kishia, Imam Ali bin Musa Ridha AS.

Haram ya mtukufu huyo iko Mash'had, kaskazini mashariki mwa Iran. Mamilioni ya wapenzi wa Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad SAW hufanya ziara kwenye haram hiyo kila mwaka kutoka kona zote za dunia.

 

 

 

4002964

captcha