IQNA

Palestina yapinga utawala wa Israel kuwa mwanachama mwangalizi Umoja wa Afrika

21:51 - February 05, 2022
Habari ID: 3474894
TEHRAN (IQNA)- Viongozi na makundi ya ukombozi wa Palestina wameutaka Umoja wa Afrika (AU) kufikiria upya uamuzi wa mwaka jana wa kuipa Israel hadhi ya kuwa mwangalizi katika umoja huo.

Wito huo wa pamoja umetolewa wakati wakuu wa nchi za Afrika wakikutana mjini Addis Ababa katika mkutano wa kilele wa siku mbili wa jumuiya hiyo yenye wanachama 55, uliofunguliwa katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa leo Jumamosi.

Waziri Mkuu wa Palestina, Mohammed Shtayyeh amesema Israel haikupaswa kamwe kupewa tuzo kwa ukiukaji wake wa haki za Wapalestina na kwa sera zake za ubaguzi wa rangi unawanyanyaza watu wa Palestina."

Mohammed Shtayyeh ameongeza kuwa anapenda kuwataarifu viongozi wa Afrika kwamba hali ya watu wa Palestina imezidi kuwa mbaya.

Mgogoro wa kutambuliwa Israel kama mwanachama mwangalizi katika Umoja wa Afrika ulianza Julai mwaka jana wakati Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, alipoupatia utawala huo haramu hadhi ya kuwa mwanachama mwangalizi katika umoja huo na kusababisha mzozo mkubwa ndani ya chombo hicho.

Mapema leo Jumamosi Faki alitetea uamuzi wake, akidai kuwa unaweza kuwa "wenzo wa kuhudumia ya amani".

Harakati za ukombozi wa Palestina zimepinga madai hayo ya Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika huku Hamas ikitoa wito kwa Waafrika wote wanaopenda uhuru kupaza sauti ya mshikamano na taifa la Palestina na kumlazimisha Faki abatilishe uamuzi wake. 

Taarifa iliyotolewa na Hamas imesema: "Utawala ghasibu wa Israel kwa muda mrefu umekuwa ukifanya ugaidi wa kiserikali na unatekeleza jinai za kimfumo dhidi ya watu wa Palestina, makazi yao na maeneo matakatifu. Unatekeleza sera ya maangamizi ya kimbari na kikaumu kama ilivyothibitishwa na mashirika mengi ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu."

Taarifa ya Hamas imeongeza kuwa: "Kutoa uanachama, japo hadhi ya kuwa mwangalizi tu kwa Israel, ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu pamoja na kanuni na sheria za AU, ambayo inapinga ubaguzi wa rangi na ukoloni.

Mkutano wa 35 wa Viongozi wa Umoja wa Afrika, AU, umeanza leo huko Addis Ababa, Ethiopia na miongoni mwa ajenda za vikao vyake ni kujadili janga la mapinduzi ya kijeshi yaliyotikisa nchi sita za Afrika Magharibi katika miezi ya karibuni, masuala ya usalama, uchumi, afya na athari mbaya za janga la maambukizi ya corona.

4033926

captcha