IQNA

Kijana msomaji Qur'ani adungwa kisu na kuuawa London

17:01 - November 09, 2021
Habari ID: 3474534
TEHRAN (IQNA)- Kijana mmoja ambaye ni imamu na msomaji Qur'ani nchini Uingereza amepoteza maisha baada ya kudungwa kisu katika eneo la Tower Hamlets mjini London.

Kwa mujibu wa taarifa, Hafidh Mohammad Aqil Mehdi, 22, alipoteza maisha Jumamosi asubuhi baada ya kudungwa kisu. Hadi sasa haijabainika sababu za ukatili huo na wala hakuna aliyekamatwa ingawa polisi wamesema wanaendeleza uchunguzi.

Afisa wa Idara ya Upelelezi Laurence Smith amesema uchunguzi uko katika hatua za awali lakini amesisitiza kuwa wana azma ya kuhakikisha haki inatendeka na waliohusika na mauaji hayo wanakamatwa. Aidha ametoa wito kwa mashahidi walioona chochote kinachoweza kusaidia katika uchunguzi kufikisha taarifa kwa idara ya upelelezi.

Marhum Mehdi alikuwa ametambulika kutokana na usomaji wake mzuri wa Qur'ani Tukufu na alikuwa akisalisha Sala ya Tarawih msikitini katika Mwezi Mtukufu Ramadhani mbali na kutoa mafunzo ya Qur'ani kwa watoto wa mtaa alimokuwa akiishi.

Mwalimu wa marhum Mehdi, Ishaaq Abu Rahmiyyah Jasat amesema amesikitishwa na kifo cha Mehdi na kumtaja kuwa mwanafunzi aliyekuwa na kipaji cha kipekee. Amesema amekuwa akimfunza kwa muda wa miaka 10 na alifanikiwa sana katika safari yake ya kujifunza Qur'ani Tukufu.

Jinai zitokanazo na hujuma za visu zimeongezeka Uingereza  kwa asilimia  35 mwaka huu.

/3476413/

captcha