IQNA

Gaddafi, Haftar wanawasiliana na Israel kupata himaya katika uchaguzi wa rais Libya

13:39 - November 19, 2021
Habari ID: 3474576
TEHRAN (IQNA)- Ripoti mpya imefichua kuwa utawala haramu wa Israel unaunga mkono wagombea wawili katika uchaguzi wa rais utakaofanyika Libya mwezi Disemba.

Gazeti la Al-Akhbar la Lebanon limefichua kuwa, utawala wa Israel unaunga mkono wagombea wawili wakuu katika uchaguzi wa rais Libya nao ni jenerali muasi Khalifa Haftar na Saiful Islam Gaddafi, mwanae mtawala wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi.

Imedokezwa kuwa wawili hao wametoa hakikisho kuwa wanaunga mkono Libya kuanzisha uhusiano na utawala wa Israel na kwa msingi huo wamepata himaya ya Tel Aviv.  Aidha gazeti hilo limedokeza kuwa utawala wa Israel unafadhilisha zaidi Haftar awe rais wa Libya kwa sababu atafanikisha malengo ya utawala huo ya kuwa na satwa kamili katika ukanda wa Bahari ya Medieterrania.

Gazeti la Al Akhbar limeandika kuwa, wagombea hao wa urais Libya wanaamini kuwa, kujikurubisha kwa Israel na kuwasaliti Wapalestina kutapelekea wapate ridhaa ya Marekani na hivyo kuimarisha uwezekano wao wa kuchaguliwa.

Al Akhbar limeandika kuwa, hivi karibuni, Saddam, mwanae Khalifa Haftar, alitembelea Tel Aviv na kukutana na maafisa wa utawala wa Israel na akawahakikishia kuwa baba yake yuko tayari kuanzisha uhusiano na utawala huo haramu.

Aidha imedokezwa kuwa Saddam kimsingi ndiye atakayekuwa mtawala wa nyuma ya pazia iwapo baba yake atashinda uchaguzi nchini Libya. Ripoti hiyo pia inasema Saif al Islam Gaddafi aliendeleza mawasiliano ya siri na Israel baada ya baba yake kuondolewa madarakani mwaka 2011. Uchaguzi mkuu wa Libya unatazamiwa kufanyika Disemba 24.

4013490

captcha