IQNA

UNESCO yatengea lugha ya Kiswahili siku maalumu kimataifa

22:53 - December 04, 2021
Habari ID: 3474641
TEHRAN (IQNA)- Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu , Sayansi na Stamaduni UNESCO limeitangaza rasmi tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa siku ya Kiswahili Duniani.

Uamuzi huo wa kihistoria umefikiwa Novemba 23 kwenye makao makuu ya UNESCO mjini Paris Ufaransa wakati wa mkutano wa nchi wanachama wa shirika hilo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa wa twitter wa UNESCO azimio maalum la kuitangaza siku hiyo limepitishwa na wanachama wote bila kupungwa.

Lugha ya kwanza Afrika

Hatua hiyo inakifanya Kiswahili kuwa lugha ya kwanza ya Kiafrika kutambuliwa na Umoja wa Mataifa na kuwa na siku maalum ya kuadhimishwa.

Kiswahili hadi sasa tayari kinatambulika kama miongoni mwa lugha rasmi kwenye Muungano wa Afrika, na kinatumika kama lugha rasmi kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki na bunge la Afrika na ni moja ya lugha za Afrika zinazozungumzwa na watu wengi duniani.

Taarifa zaidi kuhusu azimio hili na lina maanisha nini kwa wazungumzaji wa Kiswahili duniani tutakuletea katikia vipindi vyetu vijavyo.

Heshima kubwa

Wakati huo huo Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa ambaye  pia ni mwakilishi wa kudumu wa Tanzania UNESCO, Samwel Shelukindo,   amesema lugha ya Kiswahili kutambulika rasmi na UNESCO, ni heshma kubwa na tunu ya kipekee kwa wazungumzaji wa lugha hiyo.  

Akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa Balozi Shelukindo amesema mbali ya heshima kubwa pia ni fursa ya kipekee kwa wazungumzaji wa lugha hiyo ikiwa ni pamoja na fursa za ajira, biashara na kutangaza utamaduni wa Waswahili kote duniani.

Mchakato uliopelekea mafanikio

Balozi Shelukindo akifafanua kuhusu mchakato  wa kufikia hatua hiyo amesema

“Mchakato haukuanza zamani sana lakini ulianzia mbali kwani mwaka 2004 Muungano wa nchi za Afrika AU ulikipitisha Kiswahili kama moja ya lugha za kufanyia kazi, mwaka 2018 Jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika SADC ilipitisha Kiswahili vilevile kama lugha ya kufanyia kazi katika ukanda wa SADC lakini Kiswahili vilevile kimekuwa kikitumika kwa muda mrefu  na Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki na baada ya hapo serikali yetu ya Tanzania ikasema tukisongeshe mbele zaidi na ili kiende mbele zaidi lazima kitambuliwe na shirika la UNESCO la Umoja wa Mataifa na kinaanza na hatua hii ya kutengewa siku maalum ya kuadhimishwa ambayo tumepewa tarehe 7 Jualai ya kila mwaka.” 

Fursa kubwa

Na je hatua hii inamaanisha nini kwa Tanzania ambako na kwa wazungumzaji wote wa Kiswahili duniani?

“Ina maana kubwa sana na pia ni fursa kubwa sana , fursa kubwa kwa Watanzania kuanza kutumia Kiswahili katika kila nyanja za kufanya maendeleo, kwenye biashara , kwenye elimu pia kwa mfano kuanzia sasa hivi kutakuwa na mahitaji mengi sana ya waalimu wa kufundisha Kiswahili kama lugha ya kigeni, na pia mchakato ukisonga mbele hapo baadaye watu kama wakalimani pia watahitajika. Hivyo kuwa na wataalamu wa Kiswahili ni fursa kwenda hata nje ya nchi kufundisha lugha hiyo.” 

Kwa nini 7 Julai?

Balozi Shelukindo amesema imetengwa tarehe 7 Julai kwa sababu kihistoria hiyo ni tarehe muhimu sana

“Tarehe 7 Julai ndio siku Muasisi wa taifa la Tanzania hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alianza kutumia Kiswahili kama lugha ya kuwaunganisha watanzania kudai ukombozi, lakini tarehe 7 Julai mwaka 2000 Jumuiya ya Afrika Mashariki ndio ilizaliwa upya na pia tarehe 7 Julai ni sabasaba , ni biashara kwa hiyo unaona Kiswahili kilivyoingia hapo na kwamba Kiswahili sasa kitumike pia zaidi katika biashara.” 

Mkakati wa kukuza Kiswahili

Na baada ya mchakato huu wa kutangazwa na kuwa na siku maalum ya kuadhimisha lugha hiyo nini kinafuata?

Balozi Shelukindo amesema “Ninaamini sasa serikali yetu pamoja na wadau wote wa Kiswahili, ikiwemo taasisi za Kiswahili kama BAKITA, Baraza la Kiswahili la taifa , chuo kikuu cha Dar es salaam lazima sasa waje na mkakati wa namna gani ya kukikuza lakini mkakati mzuri ni kuanzia vitu kama vituo vya kufundisha Kiswahili katika nchi na sehemu mbalimbali na hapo sasa tutapata fursa zaidi ya kukikuza Kiswahili.”

Mwisho kabisa Balozi shelukindo ametoa wito kwa wapenzi na wazungumzaji wa Kiswahili kote duniani

“Kwa wazungumzaji wa Kiswahili hii ni fursa lakini pia tunajivunia na kuitumia vizuri sasa. Nadhani tuendelee kukikuza kwani hakuna sababu ya kuendelea kukaa nyuma. Lakini napenda kutoa angalizo kwamba Kiswahili sio cha kwetu tuu, hii ni lugha ya Afrika. Tusipoitumia fursa wenzetu , majirani zetu wataitumia fursa hiyo watafundisha wakalimani, watafundisha waalim na huwezi kuwaambia chochote kwa sababu wao ndio wamekipitisha.” 

Balozi pia amewataka wapenzi wa Kiswahili kote duniani kuhakikisha wanaitumia lugha hiyo na kuipeperusha kila kona ya dunia.

 

Kishikizo: kiswahili ، unesco
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha