Hussein Amir-Abdollahian amesema hayo mjini Islamabad pambizoni mwa mkutano wa Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) katika mazungumzo yake na Riyadh al-Maliki, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Palestina.
Sambamba na kusisitiza himaya na uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa wananchi wa Palestina, Hussein Amir-Abdollahian amelaani vikali jinai za utawala haramu wa Kizayuni wa Israel katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu.
Wakati huo huo, akizungumza jana katika kikao cha dharura cha Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kilichofanyika mjini Islamabad, kwa ajili ya kujadili matukio ya Afghanistan, Amir-Abdollahian alisema kuwa, amani endelevu na ya kudumu itaweza kupatikana tu nchini Afghanistan ikiwa itaundwa serikali shirikishi na itakayojumuisha pande zote.
Aidha alisema kuwa, kucheleweshwa kwa jambo hilo kutawapa fursa maadui wa Afghanistan ili sambamba na kushamirisha ugaidi wa Kidaesh, wawazidishie matatizo ya kiuchumi na hali mbaya ya maisha na ya kiafya watu wa nchi hiyo, kuwafanya washindwe kujikimu kwa mahitaji yao ya msingi ya maisha, kuustawisha upya mtandao mpana wa uhalifu wa kijamii na kuzidisha umasikini na baa la njaa baada ya miaka 20 ya nchi hiyo kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu na kuteketezwa miundomsingi yake yiote na hivyo kuwafanya viongozi na watu wake washindwe kufanya chochote.