IQNA

'Drone' ya upelelezi ya Hizbullah yaingia ardhi zinazokaliwa na Israel

20:37 - February 19, 2022
Habari ID: 3474945
TEHRAN (IQNA)- Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Lebanon ya Hizbullah imetangaza kuwa ndege yake moja isiyo na rubani au drone aina ya "Hassan" imeingia hadi ndani ya anga ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ambazo zimepachikwa jina la Israel na kutekeleza oparesheni ya kukusanya taarifa za siri.

Taarifa zinadokeza kuwa jana Ijumaa kuwa, sauti za ving'ora vya hali ya hatari zilizisikika katika vitongoji vya Kizayuni karibu na mpaka wa Lebanon hususan katika eneo la Al Jalil.

Televisheni ya Al Manar ya Lebanon imerusha hewani taarifa ya Hizbullah iliyosema kwamba ndege yake moja ya droni aina ya "Hassan" ( ya kulienzi jina la Shahidi Hassan al-Laqqis) ilipaa ndani kabisa ya anga ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu kwa muda wa dakika 40 na katika umbali wa kilomita 70; na kwamba baada ya kutekeleza operesheni ya upelelezi wa kutosha ilirejea  kituoni kwake nchini Lebanon salama usalimini.

Katika taarifa yake hiyo, Hizbullah imesisitiza kuwa licha ya kuwepo silaha na zana za ugunduzi za adui, ndege hiyo isiyo na rubani ilifanikiwa kurudi salama baada ya kukamilisha kazi yake.

Hayo yameripotiwa katika hali ambayo, jeshi la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel limekiri rasmi katika taarifa kwamba, licha ya silaha na zana zote za ugunduzi lilizonazo, likiwemo kuba la chuma, ndege za kivita na helikopta halikuweza kuigundua droni hiyo iliyotokea ardhi ya Lebanon.

Kufanikiwa ndege hiyo isiyo na rubani ya Hizbullah kuingia hadi ndani kabisa ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu kumethibitisha kwa mara nyingine tena ufanisi duni wa mtambo wa ulinzi wa anga wa utawala haramu wa Israel ujulikanao kama Kuba la Chuma.

3477860

Kishikizo: hizbullah lebanon Drone
captcha