IQNA

Muqawama

Mwanaharakati: Hatua ya Hizbullah kutetea Gaza ni kulinda heshima ya ubinadamu

21:35 - October 04, 2024
Habari ID: 3479534
IQNA - Dada yake Abbas Al-Musawi, mwanzilishi mwenza na katibu mkuu wa zamani wa Hizbullah ya Lebanon, alielezea uungaji mkono wa harakati hiyo kwa Wapalestna wa Gaza ni sawa na kutetea utu wa binadamu.

Akizungumza na Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA), Huda al-Musawi amesema wapiganaji wa Hizbullah wamesimama dhidi ya utawala wa Kizayuni na kuwaunga mkono wananchi wa Ukanda wa Gaza kwa mujibu wa wajibu wa kidini na kimaadili.

Amesema utawala wa Israel umeanzisha vita vya kila namna na vya kikatili katika eneo na harakati ya Hizbullah inakabiliana na utawala huo na kuwaunga mkono Wapalestina wa Gaza ili kutetea utu na heshima ya binadamu, akirejea Aya ya 70 ya Surah Al-Isra ya Qur'ani Tukufu inayosema. “Tumewaheshimu wana wa Adam…”

Hizbullah imekuwa ikitekeleza mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya utawala haramu wa Israel tangu mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka jana, muda mfupi baada ya utawala huo ghasibu kuanzisha hujuma ya mauaji ya halaiki dhidi ya Ukanda wa Gaza kufuatia operesheni ya kushtukiza ya wapigania ukombozi wa Palestina ambao nao pia walikuwa wakilipiza kisasi jinai za miongo saba za Israel dhidi ya Wapalestina.

Hizbullah ya Lebanon imeapa kuendeleza mashambulizi yake ya kulipiza kisasi maadamu utawala Israel unaendelea na vita vyake vya Gaza, ambavyo hadi sasa vimewauwa karibu Wapalestina 42,000 wengi wao wakiwa wanawake na watoto na wengine wengi kujeruhiwa.

Kwingineko katika matamshi yake, al-Musawi ameashiria Kongamano la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu lililofanyika mjini Tehran mwezi uliopita na kusema mkutano huo unasaidia kuimarisha umoja katika Umma wa Kiislamu.

Alisema Mwenyezi Mungu, katika Qur'ani Tukufu, anawaalika Waislamu wote kuungana, akinukuu Aya ya 103 ya Surah Al Imran, “Na shikamaneni na Kamba ya Mwenyezi Mungu, wala msitawanyike. Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu alizo kuwapa nyinyi mlipokuwa maadui, na jinsi alivyoziunganisha nyoyo zenu, na kwa neema yake mkawa ndugu.”

Alisema umoja wa Kiislamu unasaidia kuimarisha imani ya Waislamu na pia kuwawezesha kusimama dhidi ya maadui kwa nguvu zao zote.

Al-Musawi ameongeza kuwa kutokana na kongamano hilo Waislamu wote wanafahamu leo ​​kwamba lengo kuu hivi sasa katika Umma wa Kiislamu ni ukombozi wa Palestina na kurejeshwa matukufu yake kwa Waislamu.

Mkutano wa 38 wa Umoja wa Kiislamu uliandaliwa na Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu katika mji mkuu wa Iran Tehran mnamo Septemba 19-21.

Zaidi ya viongozi 200 mashuhuri wa kidini kutoka kote Iran na nchi za Kiislamu walihudhuria hafla hiyo ya siku tatu ili kubadilishana mawazo kuhusu matukio ya hivi punde katika ulimwengu wa Uislamu, ambapo suala la Palestina lilikuwa kitovu cha mijadala hiyo.

 

4238375

Habari zinazohusiana
captcha