IQNA

Waandishi wa habari wa Palestina Wapigwa risasi na Wanajeshi wa Kizayuni

19:18 - March 02, 2022
Habari ID: 3474997
TEHRAN (IQNA)- Vikosi vya utawala wa Kizayuni wa Israel jana Jumanne vimewapiga risasi na kuwajeruhi waandishi wawili wa habari wa Kipalestina katika maandamano ya amani yaliyoandaliwa katika mji wa Al-Khalil (Hebron) unaokaliwa kwa mabavu na utawa huo katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Maandamano hayo yaliandaliwa kwa mshikamano na wafungwa wa Kipalestina, ambao wamekuwa wakivumilia hali ngumu ndani ya jela za kuogofya Israel.

Vyanzo vya habari vya ndani viliripoti kuwa wanajeshi wa Israel waliyadhibiti maandamano hayo kwa kutumia risasi za chuma na kuwajeruhi waandishi wa habari Abdul Muhssen Shalaldeh na Mosaab Shawer, mkononi na mguuni mtawalia.

Wanahabari wote wawili walikimbizwa hospitalini kupata matibabu ya haraka, huku wengi wa waandamanaji wakikabiliwa na kukosa hewa kutokana na wingi wa mabomu ya machozi kupigwa.

Waandamanaji hao pia wametaka kuachiliwa mara moja kwa wafungwa wagonjwa wanaopigania maisha yao, pamoja na kuachiliwa kwa miili ya mashahidi wa Kipalestina wanaoshikiliwa na Israel.

Kwingineko, Jumuiya ya Ulaya ya kutetea na kuunga mkono Quds tukufu (Jerusalem) imetangaza kuwa katika kipindi cha mwezi mmoja, askari wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel wamevamia mji huo wa Baitul Muqaddas unaokaliwa kwa mabavu na kuwatia nguvuni Wapalestina zaidi ya 190 wakazi wa mji huo.

Hujuma na mashambulio ya askari wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Quds inayokaliwa kwa mabavu na Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan na mapigano kati yao na Wapalestina yameongezeka katika miezi ya hivi karibuni.

Jumuiya ya Waulaya waungaji mkono wa Quds imeeleza katika ripoti kuwa, katika mwezi uliopita wa Februari, Wapalestina 191, wakiwemo watoto 16 na wanawake 16 walitiwa mbaroni na askari wa utawala haramu wa Israel.

Kituo cha upashaji habari cha Palestina nacho pia kimetangaza kuhusiana na suala hilo kuwa, Wapalestina 221 wakiwemo makumi ya wanawake na watoto wamejeruhiwa katika mapigano yaliyotokea mwezi uliopita mjini Baitul Muqaddas inayokaliwa kwa mabavu.

3478017

captcha