IQNA

Jumuiya ya Waislamu huko North Carolina Marekan yatoa msaada wa chakula Ramadhani

19:09 - April 30, 2022
Habari ID: 3475190
TEHRAN (IQNA)- Kituo cha Jumuiya ya Kiislamu ya Raleigh katika jimbo la North Carolina nchini Marekani, ambacho ni msikiti na mahali pa kukutania jamii ya Waislamu, kimejitokeza ili kuhakikisha kila mtu aliyefunga anakuwa na Ramadhani yenye furaha.

Wafanyakazi wa kujitolea katika kituo hicho wanafanya kazi pamoja katika timu, kuanzia kwa mpishi jikoni hadi kwa wale wanaopakia masanduku ya chakula, ili kutoa chakula kwa watu wanaohitaji.

Mohamed Elgamal, mfanyakazi wa kujitolea na mwenyekiti wa kamati ya kijamii na ustawi katika msikiti huo, anasimamia maandalizi ya chakula na usambazaji.

"Mwezi wa Ramadhani sio tu kufunga, lakini pia ni mwezi wa kutoa," Elgamal alisema. "Ni kutoa katika jamii, kuwapa watu ambao ni wahitaji sana na kusaidia masikini."

Mahitaji ya chakula cha bure ni ya juu zaidi mwaka huu. Waislamu kutoka matabaka mbalimbali, kama vile wale wanaotoka katika kaya zenye kipato cha chini, wanafunzi na wakimbizi, wanajitokeza kwa wingi kupokea msaada.

"Kila mwaka, kwa wastani tunatoa milo 350 kwa siku. Mwaka huu ni zaidi ya milo 540,” Elgamal alisema. “Sababu ya ongezeko hilo ni mahitaji makubwa ya chakula hicho. Na pia tuna hapa katika eneo la Raleigh wakimbizi wengi kutoka Afghanistan, kutoka Syria.

Haya yote yanawezekana kutokana na michango ya ukarimu kutoka kwa jamii ya Kiislamu.

“Wanakuja na tunawahudumia. Nadhani itawasaidia pia kula chakula, chakula cha moto, kama sisi sote tunavyofanya nyumbani," Elgamal alisema. "Lakini msaada huu unahitajika sana kwa jamii."

Watu wa kujitolea wa kila rika hutoa muda na pesa zao kuhakikisha kila mwanajamii anakuwa na Ramadhani yenye baraka.

Kwa wakimbizi ambao hawana gari lao wenyewe au usafiri wa kufika msikitini, kituo hichi huwasafirisha nyumbani. Watu wa kujitolea pia hufikisha chakula kwenye nyumba za wakimbizi.

3478718

captcha