IQNA

Waislamu wa Marekani watoa dola bilioni 1.8 kupitia Zaka

10:42 - April 28, 2022
Habari ID: 3475178
TEHRAN (IQNA)- Utafiti wa hivi karibuni umebaini kuwa Waislamu wa Marekani walitoa msaada wa dola bilioni 1.8 mwaka 2021, mwaka huo huo ambao ulishuhudia ongezeko kubwa la visa vya ubaguzi na unyanyasaji dhidi ya wafuasi wa dini hiyo ya Mwenyezi Mungu.

Taasisi ya Muslim Philanthropy Initiative katika Chuo Kikuu cha Indiana imesema katika ripoti iliyotolewa wiki iliyopita kwamba, mwaka jana Wamarekani Waislamu walitoa wastani wa dola bilioni 1.8 kupitia Zaka, ambayo faradhi ya kidini.

Kulingana na ripoti hiyo, kila Mwislamu wa kawaida nchini Marekani alichangia takriban dola 2,070 za Zaka. 

Zaka ni moja ya nguzo tano za Uislamu na wajibu wa kila mwaka kwa Waislamu wote kutoa sehemu ndogo ya mapato na mali zao kwa ajili ya sadaka.

Shariq Siddiqui, Mkurugenzi wa Muslim Philanthropy Initiative, amesema kuna uwezekano mkubwa kwamba kiasi kikubwa cha dola bilioni 1.8 kilitolewa wakati wa mfungo wa mwezi wa Ramadhani ambapo malipo na thawabu za mema huzidishwa.

Ripoti hiyo imeonyesha kuwa sehemu kubwa ya Zaka hiyo ilitolewa kwa mashirika ya kimataifa yasiyo ya faida.

Sharif Aly, afisa mkuu mtendaji wa Islamic Relief USA amesema: "Ingawa Zaka ni wajibu wa kidini, lakini pia ni njia ya kushughulikia matatizo ya kijamii ambayo yameathiri watu, yamesababisha watu kuwa masikini, na kufanya maisha yao kuwa magumu." 

Wakati huo huo, kundi la kutetea Waislamu na haki za kiraia linasema, kesi za ubaguzi na unyanyasaji dhidi ya Waislamu nchini Marekani ziliongezeka kwa asilimia tisa mwaka jana ikilinganishwa na 2020.

Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani (CAIR) limesema katika ripoti iliyochapishwa Jumatatu kwamba lilipokea malalamiko 6,720 mwaka jana, na kuonya kwamba, takwimu zilizotajwa katika ripoti hiyo bado ni ndogo.

Nihad Awad, Mkurugenzi Mtendaji wa CAIR, amesema katika mkutano na waandishi wa habari kwamba chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) inafanyika kimuundo na mpangilio maalumu na kwa kina katika jamii Marekani.

4052567

Kishikizo: waislamu marekani Zaka cair
captcha