IQNA

Kiongozi Muadhamu katika mkutano na Amir wa Qatar

Inatazamiwa kuwa ulimwengu wa Kiarabu utakabiliana kisiasa na jinai za utawala wa Kizayuni

6:53 - May 13, 2022
Habari ID: 3475243
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema dhulma ya miongo kadhaa ya utawala khabithi wa Kizayuni dhidi ya watu wa Palestina ni ukweli mchungu wa historia na pigo kwa ulimwengu wa Kiislamu na Kiarabu na kuongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataraji kwamba ulimwengu wa Kiarabu utaingia wazi wazi katika medani ya kisiasa kukabiliana na jinai hizo.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo Alhamisi mjini Tehran alipokutana na Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani  na ujumbe aliokuwa ameandamana nao. Katika kikao hicho, Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa: "Muelekeo wa nchi za Kiarabu kuhusu jinai za utawala wa Kizayuni iwapo utachukuliwa kwa kuogpa au kwa kuwa na matumaini kuhusu utawala huo, basi leo nchi hizo zinapaswa kufahamu kuwa, utawala ghasibu wa Israel uko katika hali ambayo hakuna anayeweza kuwa na matumaini nao au kuuogopa."

Kiongozi Muadhamu amesema utatuzi wa masuala ya eneo unawezekana kwa mazungumzo baina ya nchi za eneo na kuongeza kuwa: "Masuala ya Syria na Yemen pia yanaweza kutatuliwa kwa mazungumzo." Amesema mazungumzo hayapaswi kuwa katika hali ya udhaifu kwani upande wa pili katika mazungumzo ambao aghalabu huwa ni Marekani na wengine hutegemea nguvu za kijeshi na kifedha.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa masuala ya eneo yanaweza kusimamiwa au kuendeshwa bila kuhitajia uingiliaji wa madola ya kigeni. Ameendelea kusema kuwa: "Wazayuni hueneza ufisadi kila mahala wanapoingiza mguu wao na hawazipi nchi zingine tahafifu na kwa msingi huo nchi za eneo zinapaswa kuimarisha uhusiano wao kadiri ziwezavyo kupitia ushirikiano na kutafakari pamoja.

Kiongozi Muadhamu pia amesisitiza kuhusu kustawishwa uhusiano wa kisiasa na kiuchumi baina ya Iran na Qatar. Aidha amesema kuimarishwa na kuwa endelevu uhusiano wa Iran na Qatar ni kwa maslahi ya nchi hizi mbili. Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa, kiwango cha sasa cha uhusiano wa kiuchumi baina ya nchi mbili kiko chini sana na kinapaswa kuongezeka maradufu  sambamba na kuainishwa muda wa kutekeleza mapatano yaliyofikiwa.

Katika kikao hicho, Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani  amebainisha furaha aliyekuwa nayo kwa kuitembelea Iran. Huku akiashiria hadhi na nafasi ya juu ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Ulimwengu wa Kiislamu amesema, jinai zinazotendwa na utawala wa Kizayuni wa Israel huko Palestina ni za kuogofya na kuna haja ya kusimama kidete kukabiliana na jinai hizo zinazotekelezwa dhidi ya Wapalestina.

Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani pia amesema njia ya kutatua masuala ya nchi za eneo kama vile Syria, Iraq na Yemen ni kupitia mazungumzo. Huku akiashiria uhusiano wa kiuchumi wa Iran na Qatar amesema:"Kamati ya uchumi baina ya nchi mbili sasa inafanya kazi na mwaka ujao ushirikiano wa kiuchumi utaongezeka kwa kiwango kikubwa."

4056572

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
* :