IQNA

Kiongozi Muadhamu katika mkutano na Amir wa Qatar:
12:12 - January 13, 2020
News ID: 3472366
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei amesema: Mazingira ya eneo yalivyo hivi sasa yanahitaji zaidi kuliko ya kabla yake kuimarishwa mawasiliano kati ya nchi za eneo na kutokubali kuathiriwa na chokochoko za maajinabi.

Ayatullah Khamenei alitoa sisitizo hilo Jumapili usiku mjini Tehran katika mkutano na Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Aal Thani pamoja na ujumbe aliofuatana nao.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, hali ya sasa ya eneo si ya kuridhisha na akaongeza kwamba: Sababu ya hali hii ni nia ovu na haribifu ya Marekani na marafiki zake; na njia pekee ya kukabiliana nayo ni kutilia mkazo mashirikiano ya ndani ya eneo.

Ameashiria pia uhusiano mzuri wa kisiasa uliopo baina ya Iran na Qatar na akasema: Uhusiano wa kibiashara kati ya nchi mbili haujafikia kiwango cha uhusiano wa kisiasa na inapasa mashirikiano kati ya Iran na Qatar katika nyanja zote za pamoja yapanuliwe zaidi ya ilivyokuwa hapo kabla.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Bila shaka kuna baadhi, na hasa wale ambao wamekuja katika eneo kutoka upande wa mbali wa dunia, ambao hawapendezwi na kustawishwa uhusiano baina ya nchi za eneo, lakini jambo hili wao haliwahusu; na nchi na mataifa ya eneo hayakubali tena udhibiti na uingiliaji wao wa aina hiyo.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Rais Hassan Rouhani, Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Aal Thani, mbali na kueleza furaha kubwa aliyokuwa nayo ya kukutana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema, hali ya eneo ni ngumu na akaongeza kwamba: Sisi tunakubaliana kikamilifu na uliyoyasema kuhusu ulazima wa kuongezwa mashirikiano ya kieneo na tunaitakidi kwamba inapasa yafanyike mazungumzo jumuishi kati ya nchi za eneo.

Wakati huo huo,

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema uhusiano wa kisiasa baina ya Iran na Qatar ni mzuri lakini nchi mbili hizo zina fursa ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili wa Doha na Tehran na katika nyuga mbalimbali zikiwemo za uchumi, biashara, utalii na sayansi.

Rais Rouhani alisema hayo jana Jumapili hapa Tehran katika kikao na waandishi wa habari akiwa pamoja na Amir wa Qatar, Tamim bin Hammad Aal Thani na kusisitiza kuwa, "Nchi fulani zimeiwekea Qatar vikwazo na kuiweka chini ya mzingiro, lakini Iran ilisimama na itaendelea kusimama na nchi hiyo ikiwa ni katika kutekeleza jukumu lake la ujirani mwema."

Dakta Rouhani amesisitiza kuwa, Iran na Qatar zina uhusiano mpana na wenye historia ndefu na kwa msingi huo, Tehran itaendelea kusimama bega ka bega na Doha katika hali zote.

Kwa upande wake, Tamim bin Hammad Aal Thani, Amir wa Qatar mbali na kupongeza uhusiano mzuri uliopo baina ya nchi mbili hizi, amesisitiza haja ya kutumika mazungumzo na diplomasia katika kuipatia ufumbuzi migogoro inayozikabili nchi za Asia Magharibi.

Amiri wa Qatar aliwasili Tehran jana alasiri na kulakiwa na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Kasri la Sa'ad Abad hapa jijini Tehran.

3871109

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: