IQNA

Vazi la Hijabu ni haki

Waislamu Nigeria wapongeza amri ya mahakama ya kuruhusu Hijabu shuleni

22:57 - June 20, 2022
Habari ID: 3475403
TEHRAN (IQNA)- Waislamu nchini Nigeria wamepongeza hukumu ya mahakama ya kilele ambayo imesema wanafunzi wa kike Waislamu wana haki ya kuvaa vazi la staha la Hijabu katika shule za serikali mjini Lagos.

Katika taarifa, Al-Haji Ibrahim Abdullahi ambaye ni mwanaharakati wa sekta ya habari amesema uamuzi wa mahakama ya kilele kuhusu hijabu muhimu sana kwani utarejesha nidhamu, amani na ustawi katika sekta ya elimu nchini humo.

Al-Haj amesema utumizi wa vazi la Hijabu unaweza kulinganishwa na vazi la watawa wa kanisa Katoliki kwani ni vazi ambalo linalinda maadili na kuongeza kuwa marufuku ya hijabu ilikuwa ni kitendo cha ubaguzi dhidi ya Waislamu sambamba na ukiukaji wa haki zao.

Hivi karibuni wanafunzi wa kike Waislamu nchini Nigeria walishinda kesi na kupata haki yao baada ya mahakama ya juu zaidi ya nchi hiyo kutoa hukumu ya kuruhusu wanafunzi wa kike wavae Hijabu bila kusumbuliwa au kubaguliwa wanapokuwa maskulini katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Watano katika ya majaji saba wa jopo maalumu la kushughulikia kesi hiyo, wamepasisha hukumu ya kuruhusiwa wanafunzi wa kike kuvaa vazi la staha la Hijab wanapokuwa shuleni ambapo majaji wawili waliosalia walijizuia kupiga kura.

Serikali ya jimbo la Lagos huko Nigeria ilikuwa imepiga marufuku matumizi ya vazi la staha la Hijab ikidai kuwa si sehemu ya sare za skui walizoidhinishiwa wanafunzi wa kike

Marufuku hiyo ilipingwa na Jumuiya ya Wanafunzi Waislamu Nigeria mwaka 2015, waliosema kuwa inakiuka haki zao za mawazo, za kidini na za elimu. Mvutano wa kisheria kuhusiana na marufuku hiyo umedumu kwa muda wa miaka saba.

Tarehe 17 Oktoba 2014, Jaji wa Mahakama Kuu ya Jimbo la Lagos, Grace Onyeabo alitoa amri kwa serikali ya jimbo hilo iondoe marufuku ya vazi hilo la staha katika skuli za msingi na sekondari za umma za jimbo hilo. Hata hivyo hukumu hiyo ilizuiwa na mahakama ya rufaa tarehe 21 Julai 2016.

Uamuzi wa hivi sasa wa mahakama hiyo ya juu zaidi nchini Nigeria hatimaye unaweza kumaliza utata huo uliowaathiri zaidi wanafunzi katika shule zisizo za kidini nchini Nigeria. Mahakama hiyo imesema, kuzuia Hijabu ni kuwabagua wanafunzi Waislamu ambao wana haki ya kikatiba ya kuzingatia vazi hilo la Kiislamu.

4065307

captcha