IQNA

Shakhsia katika Qur’ani /10

Nabii Hud; Mjumbe wa kwanza wa Mwenyezi Mungu aliyezungumza Kiarabu

21:36 - October 07, 2022
Habari ID: 3475895
TEHRAN (IQNA) – Nabii Hud (AS) alitumia zaidi ya miaka 700 kuwaongoza watu wake kwenye ukweli lakini wengi wao walikataa kuukubali ukweli.

Kisha, Mwenyezi Mungu alituma adhabu kali juu ya watu wake ambayo ilisababisha kuangamizwa kwao.

Nabii Hud (AS) alikuwa miongoni mwa wajukuu wa NabiiNuh. Kuna riwaya tofauti kuhusu maisha yake. Wengine wanasema aliishi baada ya Ibrahim (AS) na kabla ya Musa (AS). Wengine wanaamini kwamba aliishi kabla ya Ibrahim (AS). Kwa vyovyote vile ni wazi kwamba alikuwa miongoni mwa wajukuu wa Nuh (AS) lakini hakuwa miongoni mwa mitume waliokuwa wajukuu wa Ibrahim (AS).

Hud (AS) alizungumza Kiarabu na baadhi ya riwaya zinasema alikuwa mjumbe wa kwanza wa Mwenyezi Mungu aliyezungumza Kiarabu.

Imepokewa kutoka kwa Imam Ali (AS) kwamba Mitume Hud, Salih, Shuaib, na Ismail pamoja na Mtume Muhammad (SAW) walizungumza Kiarabu.

Jina la Hud limetajwa katika Quran Tukufu mara 10. Pia kuna Sura ya Kitabu kitukufu iliyopewa jina lake.

Ingawa hadithi ya Hud (AS) imesimuliwa katika Sura tofauti za Qur’ani Tukufu, hajatajwa  katika vitabu vya Turarati na Biblia vilivyoko leo.

Hud (AS) aliteuliwa kuwa Nabii wa Mwenyezi Mungu akiwa na umri wa miaka 40. Alikuwa nabii wa pili, baada ya Nuhu (AS), ambaye alipambana na ibada ya masanamu.

Baadhi wameashiria kushabihiana  Hud (AS) na Nuhu (AS), ikiwa ni pamoja na umri wake mrefu na uhakika wa kwamba inasemekana alitumia zaidi ya miaka 700 akiwaongoza watu wake.

Hud (AS) ndiye mtume aliyetumwa kwa watu wa Aad. Alipewa jukumu la kuwaalika kumwabudu Mwenyezi Mungu na kuwashauri dhidi ya kuabudu masanamu. Ingawa watu wake walimwona kuwa ni mtu wa kutegemewa na mkweli, walikataa wito wake na kuanza kumtania na kumwita mwenda wazimu.

Kwa hiyo, Mwenyezi Mungu aliwaadhibu kwa kutuma dhoruba kali. Kwa mujibu wa aya za Qur’ani Tukufu, tufani ilivuma kwa usiku saba na siku nane.

Watu wote hao walikufa isipokuwa Hud (AS) na wachache wao waliokuwa waumini.

Hud (AS) na wafuasi wake walionusurika kwenye dhoruba hiyo inasemekana walienda katika mji mtakatifu wa Makka na kukaa huko kwa maisha yao yote.

Wengine wanasema Hud (AS) alizikwa Damascus. Pia kuna baadhi ya riwaya zinazosema alizikwa ama huko Homs katika Syria ya leo au Najaf katika Iraq ya leo.

captcha