IQNA

Shakhsia katika Qur’ani/5

Jinai ya kwanza ya mwanadamu ilitendwa na Qabil

20:47 - October 23, 2022
Habari ID: 3475979
TEHRAN (IQNA) – Qabil alikuwa mtoto wa kwanza wa Adam na Hawa. Hakuwa na tatizo na kaka yake Habil lakini kiburi na husuda vilimpelekea kutenda jinai ya kwanza mauaji ya kwanza katika historia ya mwandamu.

Kwa mujibu wa simulizi, Qabil alikuwa mkulima. Alifanya dhambi kubwa kutokana na husuda yake na kiburi ambacho kilimpotosha.

Jina la Qabil  halijatajwa katika Qur’ani Tukufu.  Hatahivyo yeye na kaka yake wanaitwa “wana wa Adamu” katika Kitabu Kitakatifu. “…Na wasomee khabari za wana wawili wa Adam kwa kweli...” (Surah Al-Ma'idah, aya ya 27)

Aya za 27 hadi 31 za Surah Al-Ma'idah zinaashiria kisa cha ndugu wawili. Kwa mujibu wa aya hizo, Adam, kama Nabii wa kwanza wa Mwenyezi Mungu, alipewa jukumu na Mwenyezi Mungu kumteua Habil kama mrithi wake. Hata hivyo, Qabil hakukubali suala hilo. Ndugu hao  wawili walitakiwa watoe Sadaqa kwa Mwenyezi Mungu.  Hatahivyo Mwenyezi Mungu Mtukufu aliikataa sadaka ya Qabil na jambo hili lilizidisha  husuda na kiburi katika moyo wa Qabil.

Kwa kujiona ameshindwa, Qabil aliamua kumuua kaka yake. “ Basi nafsi yake ikampelekea kumuuwa nduguye, akamuuwa na akawa miongoni mwa wenye kukhasirika”. (Surah Al-Ma'idah, aya ya 30)

Sehemu ya hadithi hii pia imetajwa katika vitabu vitakatifu kabla ya Uislamu. Kwa mujibu wa Biblia, Qabil alitoa mazao yake ya kilimo (ngano) lakini Mungu aliikataa sadaka yake. Kisha Qabil akampeleka kaka yake jangwani na kumuua.

Pia kuna riwaya zingine zinazodai kuwa husuda ya Qabil iliamshwa kwa sababu ya mapenzi, hata hivyo, maandishi yote ya matakatifu yanataja uteuzi wa Habil kama mrithi wa baba yake kama sababu kuu.

Kuna simulizi nyingi juu ya hatima ya Qabil; suala fulani ni kwamba alifukuzwa kutoka katika ardhi yake na hakuweza kujihusisha na kilimo tena.

Baadhi ya wanahistoria wanaamini kwamba kizazi cha Qabil waliuawa wakati wa mafuriko ya Nuh kutokana na dhambi zao.

captcha