IQNA

Baraza la Fatwa la Syria lasema uhamiaji ulio hatari kwenda Ulaya ni haramu

18:21 - November 13, 2022
Habari ID: 3476083
TEHRAN (IQNA) – Baraza la Fatwa la Syria limetangaza kuwa ni haramu kwa mujibu wa sheria za Kiislamu kwa Wasyria kuhatarisha maisha na mali zao kwenda Ulaya.

Baraza hilo lilisema kusafiri kwenda nchi za Ulaya kupitia njia zisizo salama ambazo zinahusisha hatari na ukiukaji wa sheria hairuhusiwi.

"Safari yoyote ambayo si salama na ambayo msafiri anakabiliwa na vitisho vya kifo, kutoweka au kuzama baharini ni Haramu kidini na yeyote anayeanza safari hiyo ni mtenda dhambi", ilisema fatwa hiyo.

Hii ni pamoja na safari za nchi kavu ambapo kuna hatari kutokana na njaa, kiu au mashambulizi ya wanyama pori, imesema Fatwa hiyo.

Baraza hilo liliongeza kuwa wanaohusika katika kuwezesha safari hizo kama vile wasafirishaji wa binadamu pia hufanya dhambi.

Tangu kuanza kwa hujuma za wanamgambo na magaidi wanaoungwa mkono na mataifa ya kigeni nchini Syria, zaidi ya watu milioni saba wameondoka katika nchi hiyo ya Kiarabu na kuelekea nchi jirani na Ulaya.

Ingawa mtiririko wa wakimbizi wa Syria kuingia Ulaya ulipungua katika miaka ya hivi karibuni, umeshika kasi tena katika miezi ya hivi karibuni, huku mamia wakiuawa katika safari hiyo kutokana na kuzama kwenye bahari ya Mediterania au ukosefu wa chakula na maji katika misitu.

4099087

captcha