IQNA

Hali ya Bahrain

Mwanaharakati Bahrain akabiliwa na mashtaka mapya ya 'kuitusi' Israel

18:37 - November 18, 2022
Habari ID: 3476111
TEHRAN (IQNA) - Mwanaharakati wa kisiasa wa Bahrain na mtetezi wa haki za binadamu ambaye tayari anatumikia kifungo cha maisha jela ameripotiwa kulengwa na msururu wa mashtaka mapya ikiwa ni pamoja na kuutusi utawala haramu Israel unaozikoloni ardhi za Palestina.

Taarifa ya familia ya mwanaharakati mashuhuri, aitwaye Abdulhadi al-Khawaja, na mashirika ya kutetea haki za kimataifa imesema kuwa Khawaja mwenye umri wa miaka 61, ambaye alifungwa gerezani mwaka 2011 baada ya kuongoza maandamano ya kuunga mkono demokrasia Bahrain, atahukumiwa wiki ijayo kufuatia mashtaka hayo mapya.

Mashtaka hayo mapya yalisemekana kuhusishwa na maandamano ya Khawaja kuhusu hali ya Gereza la Jau nchini Bahrain ambako amekuwa akishikiliwa kwa karibu miaka 12, pamoja na uchochezi wa kupindua ufalme huo na kuitusi Israel kufuatia makubaliano ya watawala kifalme Bahrain kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel.

3481294

"Baba yangu bado anakabiliwa na mashtaka mengi kwa sababu zile zile - kwamba anasisitiza kupinga dhuluma," binti ya Khawaja, Maryam al-Khawaja alisema.

Kesi hizo mpya za kisheria zinakuja, Maryam alisema, wakati kumekuwa na miito mipya kimataifa za kuachiliwa mara moja kwa baba yake, ikiwa ni pamoja na kutokana na masuala ya afya aliyonayo baada ya kuteswa na vikosi vya usalama mwaka 2011.

"Utawala wa Bahrain umetoa jibu kwa kuzidisha maradufu kisasi chao badala ya kuitikia wito wa kuachiliwa kwake," alisisitiza.

Khawaja pia anakabiliwa na shtaka jingine kwa madai ya kuvunja kiti cha plastiki mwaka mmoja uliopita aliponyimwa haki ya kuwasiliana na binti zake akiwa gerezani.

Mwanaharakati huyo mashuhuri alinukuliwa na familia yake akisema kwamba anatarajia shtaka la nne litakalofunguliwa dhidi ya baba yake kuhusiana na maandamano yake ya kupinga kushambuliwa Sheikh Abduljalil al-Miqdad, kiongozi wa kidini wa Shia ambaye pia amefungwa, mnamo Septemba.

Zaidi ya hayo, mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yalielezea mashtaka mapya kama jaribio la kumtisha Khawaja na wafungwa wengine wanaozungumza wakiwa jela.

Sayed Ahmed Alwadaei, mkurugenzi katika Taasisi ya Haki na Demokrasia ya Bahrain (BIRD) yenye makao yake makuu nchini Uingereza, alisema mashtaka hayo yanaanzisha mwenendo hatari.

"Washirika wa Bahrain nchini Marekani na Uingereza lazima walaani hadharani unyanyasaji huu unaotekelezwa na mahakama, watoe wito wa kufuta mashtaka na kuachiliwa huru mara moja na bila masharti kwa al-Khawaja," Alwadaei alisisitiza.

Khawaja alikamatwa na kufunguliwa mashtaka Aprili 9, 2011, kama sehemu ya kampeni ya ukandamizaji ya utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Khalifa nchini Bahrain kufuatia maandamano ya kuunga mkono demokrasia katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi. Alihukumiwa kifungo cha maisha Juni 22 mwaka huo,akiwa  pamoja na wanaharakati wengine wanane.

Maandamano yamekuwa yakifanyika nchini Bahrain mara kwa mara tangu ghasia za wananchi zilipoanza katika nchi hiyo ya Kiarabu katikati ya mwezi Februari 2011.

Watu wanautaka utawala wa Al Khalifah kuachia madaraka na kuruhusu mfumo wa demokrasia unaowawakilisha wananchi wote wa Bahrain uanzishwe.

Utawala wa kiimla wa kifalme, hata hivyo, kwa msaada wa Saudi Arabia na madola ya Magharibi, umetumia mkono wa chuma kukandamizamaandamano ya wapinzani.

captcha