IQNA

Hali ya Waislamu Bahrain

Bahrain yaanzisha msako dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia Ashura ikikaribia

11:18 - August 04, 2022
Habari ID: 3475577
TEHRAN (IQNA) – Utawala wa kiimla wa Bahrain umeshadidisha ukandamizaji wake wa kikatili dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini humo kabla ya Siku ya Ashura.

Wanaharakati wa mitandao ya kijamii wamechapisha video na picha za wanajeshi wa utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Khalifa nchini Bahrain wakirandaranda katika mitaa ya mji wa kaskazini wa A'ali kushusha bendera au beramu yoyote inayohusiana na kumbukumbu ya Ashura, ambayo ni kumbukizi  ya kuuawa shahidi Imam Hussein AS, Mjukuu wa Mtume Muhammad SAW ambaye ni Imamu wa tatu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia.

Mashia nchini Bahrain kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamika kuhusu ubaguzi na kutengwa mikononi mwa utawala wa Aal Khalifa unaoungwa mkono na madola ya Magharibi na utawala wa Kizayuni wa Israel

Kwa mujibu wa mashirika ya kutetea haki za binadamu, mamlaka za Bahrain zimeweka vikwazo vizito dhidi ya uhuru wa kidini wa jamii hii ya waliowengi nchini humo tangu kuzuka kwa mwamko wa Kiislamu wa wananchi na maandamano ya nchi nzima mwaka 2011.

Maafisa wa gereza maarufu la Jau nchini Bahrain wamewazuia wafungwa kuadhimisha maombolezo ya Imam Hussein AS katika mwezi huu wa Muharram kwa kisingizio cha ukiukwaji wa taratibu.

Mpinzani wa kisiasa aliyefungwa Hussein Hilal Ahmed alisema walinzi wa magereza wamewafahamisha wafungwa kuhusu hatua za vikwazo, na kusema kwamba hawaruhusu wafungwa kuhuisa maombolezo wakati wa mwezi wa kalenda ya mwezi wa Muharram.

Sheikh Hussain al-Daihi, naibu katibu mkuu wa Jumuiya ya Kitaifa ya Kiislamu ya al-Wefaq iliyopigwa marufuku nchini Bahrain, pia alilaani vikwazo vikali vya mamlaka ya Bahrain kwa raia wa Shia na kuwazuia kushiriki katika ibada za maombolezo za Ashura.

Alisema tabia hiyo iko ndani ya mfumo wa "sera ya ubaguzi wa rangi ambayo imekuwa ikikuzwa katika miaka ya hivi karibuni."

Maandamano yamekuwa yakifanyika nchini Bahrain mara kwa mara tangu mapinduzi ya wananchi yalipoanza katikati ya Februari 2011.

Wananchi wanautaka utawala wa Aal Khalifa uachie madaraka na kuruhusu mfumo wa haki unaowawakilisha wananchi wote wa Bahrain uanzishwe.

3479973

captcha