IQNA

Tafsiri na Wafasiri wa Qur'ani Tukufu /18

Tafsir Al-Safi; Tafsiri ya Qur’ani Tukufu Inayozingatia Hadithi kutoka kwa Maasumin

23:09 - February 19, 2023
Habari ID: 3476587
TEHRAN (IQNA) – Katika Tafsir al-Safi, Mulla Muhsin Fayz (Fayd) Kashani amefasiri Aya za Qur’ani Tukufu kwa kuzingatia Hadithi kutoka kwa Maasumin (AS) ambao ni kutoka nyumba ya Mtume Muhammad (SAW).

Kwa sababu ya ufupi na ukamilifu wake, Tafsir al-Safi imekuwa ukikaribishwa na wasomi na watafiti.

Katika tafsiri hii, Fayd Kashani ametumia njia ya simulizi ya tafsiri, kwa kutumia vyanzo vya Hadith vya Shia na Sunni.

Mulla Muhsin Fayd Kashani (1598-1680 Miladia) alikuwa mwanazuoni mashuhuri katika karne ya 17 Miladia nchini Iran ambaye aliandika zaidi ya vitabu 200 katika nyanja tofauti za maarifa. Alizaliwa na kufariki katika mji wa kati wa Iran wa Kashan. Baba yake alikuwa na maktaba kubwa mjini.

Baada ya kujifunza mambo ya msingi katika mji aliozaliwa, Mulla Muhsin alikwenda katika mji wa Shiraz kusoma chini ya usimamizi wa Seyed Majed Sadeqi Bahrani na Mulla Sadra.

Alikuwa karibu sana na msoamo maarufu wa wakati huo, Mulla Sadra na baadaye akamwoa binti yake. Kwa amri ya Mulla Sadra alichagua jina la Fayz. Pia alijifunza mengi kutoka kwa Khalil Qazvini na Mohammad Saleh Mazandarani. Katika uwanja wa Hikma, alimfuata Mulla Sadra na katika Irfani alielekea kwenye mawazo ya Muhiyeddin al-Arabi.

Tafsir Al-Safi ni miongoni mwa tafsiri maarufu za Kishia za Qur’ani Tukufu. Imeandikwa kwa Kiarabu na ndani yake, Mulla Muhsin amezifasiri Aya zote za Qur’ani Tukufu zikirejelea Hadithi zinazohusiana. Kitabu hiki kina utangulizi ambamo mwandishi anatoa maoni yake na uchambuzi ambao unaweza kufichua mtazamo wake, misingi na mbinu anazozitumia katika kufasiri Qur’ani Tukufu.

Anasema matakwa ya baadhi ya marafiki zake kuhusu kuandika tafsiri ya  Qur'an Tukufu kwa kuzingatia Hadithi za Maasumin (AS) yalimsukuma kuanza kazi hiyo.

Amesema kuzifahamu na kuzifafanua aya za Qur'ani kunawezekana tu kupitia kwa Mtukufu Mtume (SAW) na Maasumin au Ahl-ul-Bayt (AS) na chochote kisichotoka kwao katika suala hili, hakitegemeki. Kushindwa kurejea maneno ya Mtukufu Mtume (SAW) na Ahl-ul-Bayt (AS) katika tafsiri ya Qur'ani ni aina ya Tafsir Bil-Ray (makisio safi ya kibinafsi), ambayo ni makosa, anasema.

Katika Tafsir al-Safi, mwandishi anaanza na jina la Sura, ikiwa ni Makki au Madani, na idadi ya aya. Kisha anazifasiri Aya za Muhkam (aya zilizo wazi kabisa ambazo ziko wazi kabisa na ambazo hakuna mkanganyiko kuzihusu). Kisha hutoa Hadith kutoka vyanzo vya kuaminika vya Shia na kisha kutoka vyanzo vya Sunni. Pia anazungumzia masuala yanayohusiana na Sha’an Nuzul (sababu ya kuteremshwa), msamiati, kusoma, n.k, na kisha kutoa Hadith kuhusu fadhila za Sura na thawabu kutokana na kuisoma. Wakati mwingine pia anachambua au kueleza kuhusu Hadithi.

Katika kuandika Tafsir al-Safi, Fayz Kashani amefaidika sana kutokana na tafsiri ya Qur’ani Tukufu inayonasibishwa na Imam Hassan al-Askari (AS) pamoja na tafsiri ya Qur’ani ya Baithawi. Anaandika kwamba katika kufasiri Surah Al-Baqarah, ametumia zaidi tafsiri inayonasibishwa na Imam Hassan al-Askari (AS). Katika kunukuu Hadithi, ametumia tafsiri nyingi na kazi nyinginezo kama vile Tafsiri ya Qomi, Tafsiri ya Ayashi, na pia tafsiri za Kafi na Majma al-Bayan.

captcha