IQNA

Waislamu na Siasa Kenya

Kiongozi wa upinzani Kenya aonya kuhusu Msikiti kutumiwa katika malumbano ya kisiasa

21:04 - January 08, 2023
Habari ID: 3476376
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Kenya amemuonya mwanasiasa maarufu Muislamu nchini humo kuhusu kuutumia Msikiti kama jukwaa la kisiasa.

Kiongozi wa chama cha ODM na muungano wa upinzani wa Azimio Raila Odinga amemuonya Waziri wa Ulinzi Aden Duale dhidi ya kutumia Msikiti huo kama jukwaa la kisiasa.

Akizungumza Ijumaa mjini Mombasa, Raila pia alimuonya Mwenyekiti wa Kitaifa wa Baraza la Kitaifa la Ushauri la Waislamu Kenya (KEMNAC) Sheikh Juma Ngao kuhusu kutumia Minbar ya Msikiti kama jukwaa la kisiasa.

"Wasiende ndani ya Msikiti na kuleta siasa ndani ya msikiti. Tunaonya Bwana Duale wakiwa na Juma Ngao," Raila alisema.

Odinga hatahivyo amekiri kuwa Sheikh Juma  Ngao ni mwanaharakati ambaye amekuwa akipinga dhulma dhidi ya Waislamu Waislamu, na kwa msingi huo Muungano wa Azimio utamuunga mkono katika harakati zake hizo.

Mkuu huyo wa upinzani amesisitiza kuwa maeneo ya ibada hayafai kutumiwa kama majukwaa ya kisiasa, akidokeza kuwa kuna maeneo ya wazi ya kutumiwa kwa hilo.

Raila, kwa mara nyingine, aliwataka Rais William Ruto na Naibu wake Rigathi Gachagua kusitisha mazungumzo yao ya kisiasa makanisani.

"Hata ninyi Ruto na Gachagua, acheni kutumia kanisa kama jukwaa la kisiasa. Tukutane nje tuzungumze siasa. Lakini kanisa na msikiti zinapaswa kusalia kuwa mahali pa ibada," alisema.

Mnamo Desemba 25, 2022, Raila alimshutumu Rais Ruto kwa kutumia makanisa vibaya, akisema mipango ya serikali inafaa kuzinduliwa katika afisi za serikali, sio makanisani.

Wakati huo huo, kiongozi huyo wa ODM alishutumu uongozi wa Kanisa la Anglikana Kenya kwa kutaka kufurahisha serikali na kupuuza mapambano dhidi ya dhuluma katika jamii.

captcha