IQNA

Waislamu Kenya

Waziri wa Ulinzi Kenya aunga mkono vazi la Hijabu

21:13 - December 21, 2022
Habari ID: 3476284
TEHRAN (IQNA)- Waziri wa Ulinzi nchini Kenya, Aden Duale Jumanne ameunga mkono vazi la Hijabu ambapo amewataka wanokerwa na wanawake wa Kiislamu kuvaa vazi hilo la stara nchini Kenya watafute nchi nyingine ya kuishi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu katika ukumbi wa Sir Ali Muslim Club mjini Nairobi, Duale alipigia upatu uvaaji wa hijab, vazi ambalo limeamrishwa na Qur'ani Tukufu.

Mwanasiasa huyo maarufu ambayo huwatetea Waislamu nchini humo mara kwa mara alionekana kuwakemea wanaokerwa na wanawake Waislamu kuvaa Hijabu.

“Kila mahali ambapo serikali inawataka Waislamu waketi iwe Iddi au sikukuu ya kitaifa, tutaheshimu utamaduni wa Waislamu kwa kuhakikisha wanawake wetu wanavalia Hijabu. Iwapo una tatizo na Hijabu na uko hapa Kenya, basi afadhali uondoke nchini kwa sababu wataendelea kuvaa,” alisema Bw Duale ambaye ni mwenyeji wa eneo la kaskazini mashariki mwa Kenya.

Vipo visa kadhaa nchini Kenya ambapo baadhi ya wanafunzi Waislamu wamekuwa wakizuiwa kuvaa Hijabu shuleni. Mara nyingi umma wa Kiislamu umekuwa ukilalamikia suala hilo na kulitaja kuwa kinyume cha katiba ya nchi hiyo. Mnamo 2016, Mahakama ya Juu ilitoa uamuzi kuwa wanafunzi Waislamu wanastahili waruhusiwe kuvalia Hijab katika shule ambazo si za Kiislamu.

4108662

captcha