IQNA

Tafsiri na Wafasiri wa Qur'ani Tukufu /17

Jawami Al-Jami; Tafsiri ya Tatu ya Qur'ani Tukufu ya Sheikh Tabarsi

20:11 - February 13, 2023
Habari ID: 3476556
TEHRAN (IQNA) – Tafsiri ya Qur'ani Tukufu ya Jawami Al-Jami ni tafsiri iliyofupishwa ya Qur'ani ambayo sifa yake kuu ni kuwa kazi ya kifasihi inayofafanua aya za Qur’ani kwa maneno mafupi na inajumuisha aya zote za Kitabu hicho Kitakatifu.

Jawami Al-Jami ni tafsiri iliyoandikwa na  Fadhl ibn Hassan Tabarsi, anayejulikana kama Sheikh Tabarasi na pia ana lakabu ya Amin al-Islam. Alikuwa mfasiri mkubwa wa Kishia wa Qur'ani Tukufu. Aliiandika tafsiri hii kwa ombi la mwanawe. Inajumuisha nukuu kutoka kwa tafsiri zake mbili za Qur'ani Tukufu  ambazo ni Majma al-Bayan na al-Kafi al-Shafi. Alianza kuiandika miaka miwili baada ya kuhitimishwa kwa tafsiri zake zilizotangulia na aliimaliza katika kipindi cha mwaka mmoja.

Kuhusu Mwandishi

Fadhl ibn Hassan Tabarsi ni mfasiri mashuhuri wa Qur'ani ambaye ni mwanachuoni wa madhehebu ya  Shia na aliishi katika karne ya 6 Hijria Qamaria. Pia alikuwa ni msimuliaji wa Hadith, Faqihi (mwanasheria wa Kiislamu) na mwanatheolojia. A’alam al-Wari pia ni miongoni mwa kazi zake kuu.

Kuhusu sababu ya kuandika Jawami Al-Jami, Sheikh Tabarsi anasema alipomaliza kuandika Majma al-Bayan inayojumuisha mafundisho na sayansi mbalimbali za Qur’ani Tukufu, alipata nakala ya kitabu Kashshaf cha Zamakhshari na kuamua kutumia nukta zake. Alifanya hivyo na akaandika kitabu Al-Kafi al-Shafi. Vitabu vyote viwili vilipokelewa vizuri sana. Kisha mwanawe Abu Nasr Hassan akamtaka aandike muhtasari wa tafsiri hizo mbili katika kitabu kimoja ili kila mtu aweze kufaidika na nukta zao.

"Ingawa nilikuwa na umri wa zaidi ya miaka 70 na lilikuwa jambo gumu kwangu kufanya, ... nilikubali na kwa baraka za Mwenyezi Mungu niliweza kuandika na kuiita Jawami Al-Jami."

 

Mbinu ya Tafsiri

Tafsiri hii haina mpangilio kama Majma al-Bayan bali ni kama Kashshaf ambayo haina jedwali la maudhui. Imefupishwa sana na moja ya sifa zake kuu ni kuwa na fasihi na inafafanua aya kwa tungo fupi.

Inajadili masuala yanayohusiana na maneno, usomaji, na nukta za kifasihi na balagha. Mwandishi amejaribu kutoa kazi sahihi na ndiyo maana inafundishwa katika seminari za Kiislamu kama miongoni mwa vitabu muhimu.

Katika tafsiri hii, kwanza kuna jina la Sura, pia inaelezwa iwapo ni Makki au Madani, idadi ya aya na ubora wa Sura. Kisha inazungumza juu ya usomaji, maneno, nukta za kisarufi na kujadili zaidi maana ya aya na kutoa maoni ya kifasiri.

Pia inataja nukta za kifasihi na balagha pamoja na zile zinazohusiana na teolojia na Fiqh. Ama kuhusu aya, kwa ufupi sana inatoa nukta za Fiqhi na kisha inampeleka msomaji kwenye Majma al-Bayan.

captcha