IQNA

Wasomaji Maarufu wa Qur'ani Tukufu /30

Rubani wa Kanada alisilimu alipomsikiliza Sheikh Muhammad Rifat akisoma Qur'ani

18:21 - April 04, 2023
Habari ID: 3476812
TEHRAN (IQNA) – Baada ya kusikia kisomo cha Qur'ani cha qari mashuhuri wa Misri Sheikh Muhammad Rifat wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, rubani mmoja wa Kanada alipendezwa na Uislamu na baadaye akaenda Misri kusilimu mbele ya msomaji huyo maarufu wa Quran Tukufu.

Muhammad Rifat alizaliwa mnamo Mei 9, 1882, huko Cairo. Alikuwa na umri wa miaka miwili tu alipopoteza uwezo wa kuona kwa sababu ya uvimbe na maambukizi, na maisha yake yalibadilika tangu hapo.

Muhammad alikuwa na nia ya kusoma Qur'ani akiwa mtoto na hivyo akafuata nyayo za familia yake, hasa baba yake, katika kujifunza Qur'ani Tukufu.

Mnamo 1934, Redio Misri ilianzishwa na alialikwa kusoma Qur'ani kama msomaji wa kwanza katika idhaa hii ya kitaifa. Kwa msingi huo Surah "Al-Fath" ilisomwa kwa mara ya kwanza na Sheikh Muhammad Rifat kwenye redio ya Misri mnamo Desemba 29, 1934.

Idhaa nyingine za dunia, ikiwa ni pamoja na Radio Berlin, Radio London, na Radio Paris, zilikuwa zikianzisha vipindi vyao vya Kiarabu kwa qiraa ya Sheikh Muhammad Rifat wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Rubani wa Kanada ambaye alikuwa akihudumu katika eneo la Sahara Magharibi na majeshi ya Uingereza wakati wa vita aliwahi kusikia kisomo cha Sheikh Rifat kilichokuwa kikitangazwa kwenye Radio London. Sauti ya Sheikh Rifat ilimuathiri sana rubani huyo hivi kwamba akawaomba marafiki zake wampe nakala ya Qur'ani Tukufu ili aisome.

Baadaye alisoma kuhusu Uislamu na Waislamu na kisha akaenda Cairo kumtafuta Sheikh Rifat na kusilimu mbele yake.

Wakati Sheikh Rifat alipokuwa akisoma Qur'ani kwenye vituo mbalimbali vya redio, qiraa yake wakati mwingi haikurekedoiwa  na, kwa hiyo, visomo ni vichache vilivyorekodiwa ambavyo vimesalia kutoka kwake.

Upungufu wa pumzi ulikuwa ni ugonjwa na tatizo ambalo Sheikh Rifat alikumbwa nalo katika miaka ya mwisho ya uhai wake, na lilimsababishia shida ya kusoma.

Mwaka 1943, upungufu wa pumzi wakati akisoma msikitini nchini Misri lilikuwa ni tukio la uchungu lililowafanya wahudhuriaji kulia kwa sababu alijaribu kuendelea na kisomo chake lakini hakuweza na alishuka pale pale kwa huzuni na watu wote walilia walipoona tukio hilo. Baada ya hapo, hakuweza tena kushiriki katika vikao vya qiraa ya Qur'ani Tukufu.

Muhammad Rifat aliaga dunia Jumatatu, Mei 9, 1950, akiwa na umri wa miaka 68.

Huu hapa usomaji wake wa Surah Al-Fajr:

3483050

captcha