Kwa mnasaba wa siku hii, Youm7 ya gazeti la kila siku la Misri katika ripoti yake limeeleza jinsi Wamisri, hata Wakristo wa nchi hiyo, walivyopenda kusikiliza qiraa au kisomo cha Qur'ani cha Sheikh Rif'at.
Wakati wa uhai wake, qari huyu maarufu alikuwa na urafiki mkubwa naa mapadre na watu mashuhuri wa Kikristo wa kanisa la Kopti. Wakristo wengi wamezungumza kwa nyakati tofauti kuhusu namna walivyovutiwa na usomaji Qur’ani wa Sheikh Rif’at.
Wakristo wa Misri walipenda sana kisomo chake hivi kwamba waliwahi kuandamana dhidi ya Redio ya Qur’an nchini baada ya qari huyo kuamua kusitisha ushirikiano wake na kituo hicho cha redio.
Sheikh Rif’at alifanya uamuzi huo mwaka wa 1939 kutokana na kutokubaliana na maafisa wa idhaa hiyo.
Hali hiyo ilisababisha wimbi la maandamano kutoka kwa Wakristo na Kanisa la Kopti ambalo liliitaka redio kumtaka qari kufikiria upya uamuzi wake, kwa mujibu wa Luis Grace, mwandishi maarufu wa habari wa Kikristo nchini Misri ambaye alikuwa mhariri mkuu wa gazeti la kila siku la Sabah al-Khayr.
Amesema Wakristo wa nchi hiyo wanapenda hasa namna Sheikh Rif’at alivyosoma Surah Maryam ya Qur'ani Tukufu.
Grace alibainisha kuwa, kwa kisomo chake cha kusisimua ambacho kiligusa mioyo ya Wamisri kutoka dini zote, Sheikh Rif’at alichukua jukumu katika kuimarisha umoja wa kitaifa.
Qari huyo mashuhuri pia alichukua jukumu kubwa katika kuhimiza Wamisri wa imani zote kushiriki katika mapinduzi maarufu dhidi ya wakoloni wa Uingereza mnamo 1919, aliongeza.
Muhammad Rif’at alizaliwa Cairo mwaka wa 1882. Muhammad alipata ulemavu wa macho akiwa na umri wa miaka miwili. Baba yake, ambaye alikuwa afisa wa polisi, alimpeleka kwenye Msikiti wa Fazil Pasha huko Cairo kuhifadhi Qur'ani Tukufu ambapo alifanikiwa kuwa hafidh kamili wa Qur’ani Tukufu kabla hajafikisha miaka kumi. Muhammad Rif’at pia alijifunza kanuni za Tajweed katika miaka michache.
Akiwa na umri wa miaka 15, alipata umaarufu kama msomaji wa Qur’ani Tukufu baada ya kusoma Surah Al-Juma katika Msikiti wa Fazil Pasha. Alikuwa msomaji wa Qur’ani kwa muda wa miaka 30 kwenye msikiti huo na watu kutoka kote Misri walikuja kusikiliza kisomo chake kizuri. Sauti yake ilitikisa nyoyo za wasikilizaji na umaarufu wake ukabakia kuwa mkubwa kiasi kwamba hapakuwa na nafasi iliyobaki msikitini au maeneo ya jirani wakati wa qiraa yake. Inasimuliwa baadhi ya watu walizimia au kupoteza dhamiri wakati wakisikiliza sauti hiyo ya kipekee. Muhammad Rif’at pia alikuwa wa kwanza kusoma Qur’ani Tukufu kwenye redio ya Misri.
Pamoja na ustadi wa usomaji wa Qur’ani, Muhammad Rif’at alikuwa na ustadi juu ya Adhana (wito wa sala) na alichukuliwa kuwa Muadhini bora zaidi. Aliadhini kwa uzuri sana kiasi kwamba wengi walisilimu baada ya kusikia Adhana yake.
Sheikh Muhammad Rif’at alifariki dunia tarehe 9 Mei 1948, baada ya kuugua kwa muda mrefu, lakini usomaji wake bora wa Qur’ani unasalia kuwa wa kutia moyo muda mrefu baada ya kifo chake.
4215123