IQNA

Diplomasia

Rais Putin asema Russia iko tayari kushirikiaina kibiashara na nchi za Kiislamu

20:28 - May 19, 2023
Habari ID: 3477019
TEHRAN (IQNA)-Rais wa Russia ametangaza utayarifu wa nchi hiyo wa kuwa na ushirikiano mkubwa wa kibiashara na kiutamaduni na nchi za Kiislamu.

Rais wa Russia Vladimir Putin ametangaza katika ujumbe wake kwa washiriki wa Kongamano la 14 la Kimataifa la Uchumi "Jukwaa la Kazan: Russia - Ulimwengu wa Kiislamu" kwamba Ulimwengu wa Kiislamu unastawi ipasavyo na umepata mafanikio muhimu katika biashara, masuala ya fedha, uvumbuzi na utafiti wa kisayansi.

Putin amesema, Russia iko tayari kwa ajili ya ushirikiano mkubwa wa kibiashara na kiutamaduni na nchi za Kiislamu, kuimarisha uhusiano uliopo na kutafuta washirika wapya, na inapenda kukuza ushirikiano wa kilimo na viwanda na kuunda mitandao mipya ya usafirishaji.

Putin amesisitiza kuwa, mahusiano haya yanatokana na ushirikiano, kuheshiwa mamlaka na utambulisho wa ustaarabu wa kila upande. amesisitiza kuwa: "Tuna nia ya pamoja ya kuunda mfumo wa ulimwengu wa kambi kadhaa wa kiadilifu zaidi unaotegemea sheria za kimataifa."

Vilevile ameashiria nafasi muhimu ya Waislamu wa Russia katika kupanua mahusiano ya kimataifa na akasema, kufanyika kongamano kama hili ni uthibitisho wa ukweli huu.

Putin ameongeza kuwa "Nina imani kwamba shughuli za Kundi la Maono ya Kimkakati la Russia na Ulimwengu wa Kiislamu na Jukwaa la Kiuchumi la Kimataifa la Kazan zitaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya wafanyabiashara wa Russia na nchi za Kiislamu na kuunda fursa mpya za miradi ya pamoja.

"Russia na Ulimwengu wa Kiislamu" ni jukwaa kuu la ushirikiano wa kiuchumi kati ya Shirikisho la Urusi na nchi za Ulimwengu wa Kiislamu, na madhumuni yake ni kuimarisha uhusiano wa kibiashara, kiuchumi, kisayansi, kiufundi, kijamii na kiutamaduni kati ya Russia na nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC).

3483608

captcha