IQNA

Umra 1445

Tahadhari ya Saudia kuhusu mawakala wa Umra wasio na leseni

11:58 - August 18, 2023
Habari ID: 3477457
TEHRAN (IQNA) – Waislamu wanaokwenda Saudi Arabia kwa ajili ya Umra au Hija ndogo wameonywa dhidi ya kutumia mawakala wasio na leseni.

"Kutumia makampuni yenye leseni huhakikisha haki zako," Wizara ya Hija na Umra ya Saudi ilisema, ikihutubia wanaotaka kutekeleza ibada ya Umra

Wizara iliwashauri kuingia kwenye tovuti yake na kuangalia orodha ya mawakala walio na leseni katika nchi zao kupitia kiungo https://eservices.haj.gov.sa

Saudi Arabia inatarajia Waislamu wapatao milioni 10 kutoka nje ya nchi kufanya Umra katika msimu huu.

Msimu huu wa Umrah ulianza mwezi moja uliopita tarehe Mosi Muharram, sawa na mwanzo wa mwaka mpya wa Kiislamu wa Hijri.

Msimu huo ulianza baada ya kumalizika kwa Ibada ya Hija ya kila mwaka ambayo Waislamu wapatao milioni 1.8 walihudhuria kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mitatu baada ya vizuizi vinavyohusiana na janga la corona kuondolewa.

Waislamu, ambao hawawezi kumudu Hajj kimwili au kifedha, huenda Saudi Arabia kufanya Umra katika Msikiti Mkuu, eneo takatifu zaidi la Uislamu huko Makka.

Katika miezi ya hivi karibuni, huduma nyingi zimezinduliwa kwa Waislamu wa ng'ambo kuja nchini kufanya Umra.

Waislamu walio na aina tofauti za viza za kuingia kama vile za kibinafsi, za kutembelea na za kitalii wanaruhusiwa kufanya Umra na kutembelea Al Rawda Al Sharifa, lilipo kaburi la Mtume Muhammad (SAW) katika Msikiti wa Mtume Madina baada ya kuwasilisha ombi kwa njia ya intaneti..

Mamlaka ya Saudia imeongeza muda wa visa ya Umra kutoka siku 30 hadi 90 na kuruhusu wenye visa kuingia katika ufalme huo kupitia njia zote za ardhini, anga na baharini na kuondoka kutoka uwanja wowote wa ndege.

Ufalme huo pia umesema kuwa wahamiaji wanaoishi katika nchi za Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi wanastahili kuomba visa ya kitalii, bila kujali taaluma yao, ili kuweza kutekeleza ibada ya Umra.

Habari zinazohusiana
captcha