IQNA

Saudi Arabia kuamua kuhusu Hija mwaka huu 'katika kipindi cha wiki moja'

20:09 - June 13, 2020
Habari ID: 3472862
TEHRAN (IQNA) - Saudi Arabia inatafakari kufuta ibada ya Hija mwaka huu kutokana na kuenea janga la corona au COVID-19.

Baada ya kufutwa mijimuiko mikubwa duniani mwaka huu hasa Michezo ya Olimpiki ya Tokyo 2020, wakuu wa Saudia sasa wanatafakari kufuta Ibada ya Hija mwaka huu au kupunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya watakaotekeleza Ibada ya Hija ambayo huhudhuriwa na takribani watu milioni mbili kwa mwaka.

Afisa mwandamizi wa Wizara ya Hija na Umrah ameliambia gazeti la Financial Times kuwa Ufalme wa Saudia unatafakari masuala mbali mbali na kwamba 'uamuzi utachukuliwa katika kipindi cha wiki moja.'

Ibada ya Hija mwaka huu inatazamiwa kufanyika baina ya Julai 29 hadi Agosti 4 lakini hadi sasa wakuu wa Saudia bado hawajaondoa marufuku ya safari za ndege za kimataifa ambayo ilianza kutekelezwa Mei 20. Baadhi ya nchi kama India na Indonesia zimetangaza kuwa hazitawaruhusu wananchi wao kutekeleza Ibada ya Hija kutokana na kuenea ugonjwa wa COVID-19.

Idadi ya walioambukizwa COVID-19 imeongezeka sana Saudia baada ya serikali kuondoa vizingiti ilivyokuwa imeweka kuzuia kuena ugonjwa huo.Hadi kufikia leo Juni 13, idadi ya walioambukizwa COVID-19 nchini Saudia ni 123,000 na waliopoteza maisha ni 932.

Kufutwa ibada ya Hija kunatarajiwa kuisababishia Saudia hasara kubwa ya kiuchumi hasa wakati huu ambapo bei ya mafuta imeporomoka duniani. Gazeti la Financial Times limeandika pato la Saudia kutokana na Ibada ya Hija na Umrha ni takribani dola bilioni 12 kwa mwaka.

Wizara ya Hija ya Saudia hadi sasa haijatoa taarifa kuhusu uamuzi wa Ibada ya Hija mwaka huu. Mwezi Aprili Wizara ya Hija ya Saudia iliwataka Waislamu wasitishe mipango ya Hija hadi muelekeo wa maambukizi ya COVID-19 utakapobainika vyema.

3471672

 

Kishikizo: hija saudi arabia
captcha