IQNA

Arbaeen 1446

Wanachama wa Msafara wa Qur’ani wa Arbaeen wa Iran washiriki hafla huko Kut

22:54 - August 17, 2024
Habari ID: 3479291
IQNA - Kundi la kwanza la wajumbe wa Msafara wa Qur'ani wa Arbaeen wa Iran, unaojulikana kama Msafara wa Nur, waliandaa duru ya kwanza ya Qur'ani ya Arbaeen mwaka huu katika mji wa Kut, mashariki mwa Iraq.

Walikuwa wameondoka Iran kuelekea Iraq siku ya Alhamisi na kuzuru Haram takatifu ya Imam Ali (AS) huko Najaf kabla ya kuondoka kuelekea Kut.

Huko, walishiriki  hafla ya kwanza ya Qur'ani ya Arbaeen mwaka huu kwa ushirikiano na Jumuiya ya Mahusiano ya Qur'ani ya Iraq na ofisi yake huko Kut.

Wajumbe wa msafara huo, Mehdi Adeli na Seyed Mohammad Kermani, walisoma aya za Qur'ani Tukufu wakati wa kipindi hicho kilichorushwa na idhaa kadhaa za televisheni za Iraq.

Kwa mujibu wa Seyed Mohammad Moojani, Mkuu wa Kamati ya Qur'ani ya Makao Makuu ya Arbaeen ya Iran, msafara huo wa Qur'ani wa Arbaeen unajumuisha Wairani 98 na raia wa kigeni 34 kutoka nchi 14, kama vile Afghanistan, Tajikistan, Nigeria, India na Pakistsan.

Shughuli za msafara huo zitadumu kwa siku 12, Moojani alisema mapema.

Wasomaji wa Qur’ani kiume na wa kike pamoja na wanachama wa vikundi vya Tawasheeh watashiriki katika hafla   mbalimbali kwenye njia tofauti kuelekea Karbala wakati wa msimu wa Arbaeen, alisema.

Programu hizo zitahitimishwa kwa duru ya Qur'ani huko Karbala katika mkesha wa Arbaeen, aliongeza.

"Kwa kuzingatia matukio ya hivi karibuni huko Palestina na Gaza, programu za Qur'ani za mwaka huu zinazingatia suala la Palestina na kuwakumbuka mashahidi wa Gaza, haswa Shahidi Ismail Haniyeh," ameongeza.

Mjumuiko wa maombolezo ya Arbaeen ni mojawapo ya mikusanyiko mikubwa ya kidini duniani.

Maadhimisho ya Arbaeen hufanyika siku ya 40 baada ya Ashura, ukumbusho adhimu wa kuuawa shahidi Imam Hussein (AS), mjukuu  wa Mtume Muhammad (SAW) ambaye aliuawa shahdi na jeshi katili la la Yazid katika vita vya Karbala mwaka 61 Hijria sawa na 680 Miladia.

Kila mwaka mamilioni ya Mashia na pia idadi kubwa ya wasiokuwa Mashia humiminika  katika mji Karbala nchini Iraq, mji ulipo Haram Tukufu ya Imam Hussein (AS) ili kushiriki katika shughuli za maombolezo. Wafanya ziara, hasa kutoka Iraq na Iran, husafiri mamia ya kilomita kwa miguu hadi mji mtakatifu wa Karbala. Arbaeen ya mwaka huu inatarajiwa kuanguka mnamo Agosti 25, kulingana na kuonekana kwa mwezi.

Harakati ya mapambano ya Imam Hussein (AS) dhidi ya dhulma na ufisadi wa utawala wa Bani Umayya ilijaa hamasa, kujitolea na kusabilia kila kitu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, haki na uadilifu, na kwa sababu hiyo imegusa sana nyoyo za Waislamu na hata wapenda haki na kweli wasio Waislamu. Harakati hiyo ya Imam Hussein (AS) inaendelea kuibua vuguvugu na hamasa ya aina yake ndani ya nafsi za wapenzi wa mtukufu huyo.

3489526

 

captcha