IQNA

Mamlaka za Uingereza zamfungulia mashtaka aliyehusika na mpango wa kushambulia Misikiti ya London

7:52 - July 17, 2026
Habari ID: 3482495
IQNA – Mamlaka za Uingereza zimemfungulia mashtaka kijana mmoja kufuatia uchunguzi wa njama zilizodaiwa kuwa zililenga kushambulia misikiti katika jiji la London.

Kijana mwenye umri wa miaka 14, aliyekamatwa na polisi wa Uingereza, ameshtakiwa kwa makosa yanayohusiana na “ugaidi” kufuatia njama zilizokusudiwa kulenga misikiti ya eneo hilo.

Polisi wa Jiji la London (Metropolitan Police) walibainisha mashtaka hayo dhidi ya kijana huyo ambaye jina lake limehifadhiwa, siku ya Jumatano. Walisema kuwa kijana huyo alishukiwa kujiandaa kutekeleza “kitendo cha kigaidi” kinachohusiana na itikadi kali za mrengo wa kulia.

“Hili ni shtaka zito sana la ugaidi dhidi ya kijana mdogo, na ni jambo linalotarajiwa kuleta wasiwasi mkubwa kwa umma na jamii ya eneo hilo,” alisema Helen Flanagan, mkuu wa kitengo cha polisi cha kupambana na ugaidi jijini London.

Polisi walisema hawadhani kuwa tukio hilo linaashiria tishio pana zaidi, lakini waliongeza kuwa wamewasiliana na misikiti hiyo, iliyoko katika eneo la Sutton kusini mwa London, na kutoa ushauri na himaya.

“Tunafahamu kuwa hili litakuwa jambo la kutia wasiwasi hasa kwa jamii ya Waislamu, na tunashirikiana kwa karibu na vituo vilivyoathirika ili kuhakikisha wanapewa taarifa za hivi karibuni, na kutoa ushauri, himaya na uhakikisho, na hili litaendelea,” alisema Flanagan.

Polisi wa Uingereza walimkamata kijana huyo kwa mara ya kwanza mnamo Julai 9 kwa tuhuma za uharibifu wa gari, lakini uchunguzi wa baadaye ulibaini nyaraka zilizopelekea kushtakiwa kwa “mwenendo wa maandalizi ya kutekeleza nia ya kufanya vitendo vya kigaidi,” ilisema Polisi ya London.

Mtuhumiwa anatazamiwa kufikishwa katika mahakama ya mahakimu jijini London siku ya Alhamisi.

Tukio hili ni la hivi punde zaidi kati ya njama kadhaa zilizodaiwa au mashambulizi yanayolenga Waislamu nchini Uingereza.

Mapema wiki hii, polisi wa Uingereza waliwakamata watu 12 kuhusiana na njama za “mrengo mkali wa kulia” zilizolenga mkusanyiko wa Kiislamu uliofanyika Suffolk, mashariki mwa Uingereza.

Mwezi uliopita, mwanamume mmoja alishtakiwa kwa jaribio la mauaji yanayohusiana na “ugaidi” baada ya kufanya shambulio linaloshukiwa kuwa la chuki dhidi ya Uislamu kwa kuchoma watu visu jijini Edinburgh, Scotland.

Mkuu wa Upelelezi, Nick Blackburn, anayesimamia polisi katika eneo la kusini mwa London, alisema mamlaka zitafanya kazi kutoa “uhakikisho na himaya” kwa jamii ya Waislamu wa eneo hilo baada ya kukamatwa huko kwa hivi karibuni.

“Hatupaswi kudharau athari za mlimbikizo wa matukio ya aina hii kwa jamii ya Waislamu,” alisema.

3498285

Kishikizo: uingereza waislamu
captcha